Habari Mseto

Wanafunzi wa TUM walia bei ya vyakula kupandishwa

September 17th, 2019 3 min read

 

NA STEVE MOKAYA

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa (TUM) wameghadhabishwa na hatua ya wenye mikahawa iliyo karibu na chuo hicho kuongeza bei za vyakula.

Wanafunzi hao ambao wamekuwa katika likizo ndefu tangu mwezi Mei mwaka huu walirejea chuoni mapema mwezi huu na kupata mabadiliko katika bei za vyakula katika mikahawa hiyo.

Mbali na kuongezwa kwa bei za chakula, wanafunzi hao pia wamenungunikia kupunguzwa kwa viwango vya vyakula vinavyouzwa. Lalama hizi zimeibua mvuto wa aina yake miongoni mwa wanafunzi, kiasi cha kupelekea wengine wao kutaka kuandamana ili kulalamikia hatua hii.

Kabla ya kufunguliwa kwa chuo hicho mwezi huu, wenye mikahwa katika eneo la Tudor, kuliko chuo hicho cha TUM, walikuwa na mkutano, ambako waliamua kuangazia upya bei za vyakula. Katika mkutano huo, walikubaliana kuuza vyakula kwa bei moja na kiwango sawa.

Hivyo basi, bei za baadhi za vyakula vya kimsingi kwa wanafunzi kama vile ugali, pojo, wali na maharagwe iliongezwa. Ila hatua hii haijaenda sawa na wanafunzi , kwani wamekuwa wakilalamika wazi wazi, wakiita ‘dhuluma’.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo Dijitali ulibaini kuwa mikahawa hiyo imeongeza bei za baadhi ya vyakula. Kwa mfano, bei ya pojo, ama dengu, na maharagwe imeongezeka kutoka Sh20

hadi Sh30.

Kadhalika, bei ya ugali imepandishwa kwa Sh10, kutoka Sh30. Wanafunzi tuliozungumza nao wanasema kuwa bei hizi zimesalia kuwa za kawaida kwa muda mrefu, na hakukuwa na haja yazo kubadilishwa. Kadhalika, John Okelo, mmoja wa wamiliki wa mikahwa hiyo amesema kuwa ni kweli kwa muda wa karibu mwongo mmoja, bei hizo zilikuwa zimesimama.

Kufuatia hatua hii, sasa wengi wa wanafunzi wamelazimika kutafuta mbinu mbadala za kushibisha matumbo yao.

Wengine, hasa wanafunzi wa mwaka wa kwanza, wameamua kununua chakula chao katika mkahawa rasmi wa shule, almaarufu kama ‘mess’ ambako bei ni za chini kuliko kokote kule. Wengine wameacha kula chakula katika mikahawa, huku wakila tu kutoka nyumbani mwao.

Carol Gakii ni mmoja wa wanafunzi hao. “Nilienda ‘Maambuzi’ siku moja nikashtuka kupewa kiasi kidogo sana cha maharage,” anasema. “Sasa sidhani nitakuwa nikukula huko tena, badala yake, nitakula kutoka nyumbani tu,” anaongeza.

Duncan Chengole, kadhalika, anasema kuwa sasa imebidi awe akila akiwa nyumbani kwake tu, ama katika mikahawa iliyo mbali na chuo.

“Sasa nitakuwa nikila hapa ‘students’ center’, kwangu, ama huko katika mikahawa ya Tononoka,” anaeleza. Kwa upande wao, wenye mikahawa hii wametetea hatua yao kwa kusema kuwa hali ya maisha imepanda, na kupelekea bei za vyakula hivi kupanda kwenye masoko. John Okelo, ni mmiliki wa mkahawa wa ‘Maambuzi’.

“Kiangazi kilicho nchini kilipelekea uhaba wa vyakula hivi sokoni. Sasa ni vigumu kupata nafaka na vyakula vingine. Hii imepelekea bei ya sokoni kupanda, na hivyo kutulazimisha kupandisha bei, na kupunguza kiwango cha chakula,”anasema.

Hata hivyo, Okelo anasema kuwa wamepata malalamishi mengi kutoka kwenye wanafunzi wa chuoni, kwani wao ndio wateja wakuu. Kufuatia malalamishi hayo, amesema kuwa mkahawa wake umechukua hatua za haraka ili kudhibiti hali.

“Sasa tumeona kuwa watoto hawaji wengi kama kitambo. Wengine wao wameanza kuenda kwenye vibanda vibovu ambako hakuna usafi wa kutosha. Hivyo sasa tukaamua kurudisha bei za nafaka kama hapo awali, ila tukapunguza kiwango chao,” anasema.

Kwa upande mwingine, Alex Muge, ambaye ndiye anayemiliki mkahawa wa ‘Comrades’ Corner’, anasema kuwa wanafunzi hawafai tu kuangalia bei ya chakula, bali ubora wake.

Anasema kuwa mkahawa wake huuza baadhi ya chakula kitamu na kizuri zaidi huku chuoni, na hivyo bei hizo ni sawa. Pia yeye anatilia mkazo hoja ya kupanda kwa gharama ya maisha, iliyowalazimu kuchukua hatua hiyo.

“Ni lazima nipate faida kutokana na biashara hii. Ni lazima nilipe wafanyakazi wangu. Na ni lazima nilipe ‘bills’ zangu,”anasema.

Kadhalika, anasema kuwa amesikia malalamishi kutoka kwa wanafunzi, na hata fununu za maandamanao dhidi yao, ila anao ujumbe kwa wanafunzi.

“Sidhani kuwa ni jambo zuri kwa wanafunzi kupanga kuendakuandamana kwenye biashara za watu kwa sababu ya bei.

Badala yake, ikiwa mtu hajafurahishwa na bei ya mkahawa fulani, anaweza kuamua kutoenda huko,” anasema. Dennis Okang’a, ambaye ni kiongozi wa wanafunzi chuoni TUM, anasema kuwa pia yeye alishtushwa na hatua hiyo.

Alisema kuwa tayari ameongea na wamiliki wa mikahawa hiyo ili warudishe bei na viwango vya awali vya chakula, la sivyo, atawaomba wanafunzi wagome dhidi ya mikahawa hiyo.

“Tumewapa hadi mwisho wa mwezi huu, ikiwa hawatakuwa wameshusha bei hizo, uongozi wangu hautakuwa na linguine ila kuwaomba wanafunzi wagomee hivyo vyakula vyao watakula hayo mharagwe peke yao,” Okang’a alisema.

Wakati huo huo, imebainika kuwa wanafunzi wa TUM hawajaridhishwa na sheria mpya zilizowekwa na usimamizi wa chuo, kuambatana na masomo.

Katika sheria hizo mpya, mwanafunzi yeyote hawezi kusonga mbele katika hatua nyingine ya masomo, ikiwa ako na shida za kimasomo za mwaka uliotangulia. Kwa mfano, yeyote aliye na alama ya ‘E’ kwa somo lolote anatakikana kurudia somo hilo kwa muhula mmoja.

Jambo hili limewakera wanafunzi wengi, na sasa kuna fununu za mgomo dhidi ya hatua hii.

Katika mahojiano na Taifa Leo Dijitali , Bw Okang’a ameulaumu usimamizi wa chuo kwa kuchukua hatua pasi kuangazia athari zitakozoletwa na nazo. Ila akasema kuwa angepatana na usimamizi wa chuo ili walijadili suala hilo, kabla maji hayajazidi unga.

Kufikia wakati wa kuandikwa kwa taarifa hii, hakuna mawasiliano yoyote yaliyokuwa yamefanywa kuhusiana na mkutano huo.

Sasa imesalia kungoja ili ibainike wazi nani atakayeinamishwa na shinikizo hili kali; kati ya wenye mikahawa na wanafunzi, na usimamizi wa chuo na wanafunzi.