Kimataifa

Wanafunzi wachunguzwa kwa kufanyia chakula cha walimu 'makubwa'

May 21st, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

POLISI nchini Marekani wanachunguza kisa ambapo wanafunzi wa shule moja wanaoshukiwa kuwa walikojolea, wakatemea mate na kumwagia ‘uchafu wa ngono’ chakula cha walimu kabla ya kuwapelekea.

Wanafunzi hao wa shule iliyoko jimbo la Ohio wanasemekana kutia uchafu huo pamoja na mkojo katika vyakula aina ya ‘Crepes’, kisha wakawapelekea walimu, katika shule ya Hyatts Middle School, eneo la Powell.

Wanafunzi hao walikuwa wameandaa chakula hicho kama sehemu ya somo la kufunga mwaka, katika darasa la ekonomia.

“Mwanafunzi fulani alichukua kanda ya video wenzake wakifanya hivyo, video ambayo ilisambaa na kwa bahati mbaya wasimamizi wa shule wakaiona,” akasema Tracy Whited, mkuu wa polisi eneo hilo.

Video hiyo inasemekana kuonyesha wanafunzi wakitia mkojo na manii katika chakula hicho.

Angalau wanafunzi wanane wanahojiwa na polisi kuhusiana na kisa hicho, ambacho kinasemekana kiliwalenga walimu watano.

Polisi wanasema wanafunzi watakaopatikana na hatia ya kutia uchafu huo kwenye chakula watafunguliwa mashtaka.

Polisi aidha wamesema kuwa watafanya uchunguzi wa kisayansi kwa ‘Crepes’ hizo, ili kubaini waliotia mkojo na manii ndani yake.

“Njia muafaka ya kubaini kilichofanyika tu ni kwa kupata matokeo kutoka kwa maabara,” akasema Whited.