Wanafunzi wakorofi shuleni kunyimwa nafasi za ajira wakihitimu

Wanafunzi wakorofi shuleni kunyimwa nafasi za ajira wakihitimu

Na CHARLES WASONGA

REKODI za nidhamu za wanafunzi wanapokuwa shuleni kuanzia msingi hadi chuo kikuu zitaanza kutumika katika utoaji wa Vyeti vya Tabia Njema, Idara ya Upelelezi (DCI) imetangaza.

Vyeti hivyo huitishwa na waajiri wa kampuni za kibinafsi, mashirika pamoja na serikali kwa wale wanaoomba kuajiriwa kazi kuanzia ngazi za chini hadi za juu.

Wanaotaka kugombea nyadhifa mbalimbali za kisiasa pia huhitajika kuwa na vyeti hivyo.

Kulingana na Mkurugenzi wa DCI, George Kinoti, hatua hii ni katika juhudi za kukabiliana na ongezeko la utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi hasa migomo na uharibifu wa mali.

“Hii itakuwa ni rekodi ya kudumu ya uhalifu ambayo itazuia wanafunzi watakaoshiriki uhalifu kutimiza ndoto zao maishani, kwani hakuna mwajiri atakayekubali kuajiri kazi vijana walio na rekodi ya uhalifu,” Bw Kinoti akaeleza kwenye mtandao wa Twitter.

Bw Kinoti alisema afisi yake inakusanya maelezo kuhusu wanafunzi wa shule za msingi, upili na vyuo vikuu wanaoshiriki ama kuchochea migomo na uharibifu wa mali shuleni kwa lengo la kuwachukulia hatua za kisheria.

“Hili ni onyo kwa wanafunzi wote katika shule za msingi, upili, vyuo vya kadri na vyuo vikuu kwamba DCI inakusanya maelezo ambayo yatatumiwa kushtaki kila mmoja ambaye atashiriki vitendo vya uhalifu,’ Bw Kinoti alionya.

Vile vile, aliwataka wazazi, walezi na viongozi wa kidini kujitwika wajibu wa kutoa ushauri kwa wanafunzi ili wajiepushe na mienendo mibaya wakiwa shuleni.

Onyo la Bw Kinoti linajiri wakati ambapo visa vya migomo na uteketezaji mali za shule vinaendelea kushuhudiwa katika shule kadhaa za upili nchini.

Eneo la Nyanza ndio limeathirika zaidi baada ya shule sita kufungwa katika kipindi cha wiki moja iliyopita.

Shule zilizoathiri ni pamoja na Kisumu Girls High, Maranda Boys, Ng’iya Girls, Otieno Oyoo, Maliera High na Ambira High.

Shule ya Upili ya Chalbi iliyoko Kaunti ya Marsabit nayo ilifungwa wiki jana baada ya wanafunzi kuwashambulia walimu kadhaa wasio wenyeji wa maeneo hayo.

Nayo shule ya Upili ya Wavulana ya Thuura iliyoko kaunti ya Meru ilifungwa kutokana na visa vitatu vya uteketezaji wa mabweni.

Mnamo Ijumaa wiki jana, wanafunzi watano wa shule hiyo, iliyoko katika eneo bunge la Imenti Kaskazini, walifikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kosa la kuchoma shule kimakusukudi.

Kufuatia onyo la Bw Kinoti, huenda watano hao wajumuisha kwenye orodha ambayo idara yake inaandaa ya wanafunzi wahalifu ambao itakuwa vigumu kwao kupata Vyeti vya Tabia Njema.

Walimu wakuu na maafisa wa elimu wanasema fujo hizo zinasababishwa na kile wanachotaja kama ‘uwoga’ wa mitihani ya mwigo ambao hufanywa katika muhula huu wa pili.

You can share this post!

Wito kwa jamii ya Wakamba iitishe matangi ya maji kama...

Binti mwenye ‘nguvu za kishetani’ afukuzwa...

adminleo