Kimataifa

Wanafunzi wakusanywa kushuhudia walanguzi wa mihadarati wakiuawa

July 11th, 2018 1 min read

Na MASHIRIKA

HAINAN, UCHINA

MAMIA ya wanafunzi walikusanywa kwenda kushuhudia mauaji ya walanguzi wawili wa dawa za kulevya.

Video iliyosambazwa mitandaoni ilionyesha maafisa wa polisi wakipeleka walanguzi hao wa mihadarati katika uwanja wa michezo ulio Haikou, kusini mwa Mkoa wa Hainan, Uchina, kisha wakapigwa risasi mbele ya umati mkubwa uliojumuisha wanafunzi waliokuwa wamevaa sare za shule mbalimbali.

Kwa mujibu wa mashirika ya habari, mauaji hayo yalifanywa baada ya ruhusa kutolewa na Mahakama ya Qiongshan na Mahakama Ndogo ya Wananchi ya Haikou, kufuatia hukumu iliyotoka katika Mahakama ya Juu.

Ilisemekana kwamba ilikuwa ni sehemu ya hamasisho ya serikali kuhusu juhudi za kupambana na ulanguzi na utumizi wa dawa za kulevya, katika Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya ambayo hufanyika Juni 26 kila mwaka.

Wahalifu hao walitambuliwa kama Cai Liqun, 39, na Huang Zhengye, 36, ambao walipatikana na hatia ya kuuza dawa tofauti za kulevya katika mwaka wa 2015.

Ripoti zilisema Uchina hutekeleza hukumu kama hizo hadharani ili kutoa funzo kwa umma kuhusu athari za uhalifu.

-Imekusanywa na Valentine Obara