Habari Mseto

Wanafunzi walalamikia mmoja wao kunajisiwa

December 9th, 2020 1 min read

Na BRIAN OJAMAA

WANAFUNZI wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Lugulu, Kaunti ya Bungoma jana walifanya maandamano kulalamikia kubakwa kwa mmoja wao.

Walidai kuwa mwenzao alibakwa mnamo Jumamosi alfajiri katika bafu ya bweni la Muliro alipokuwa akioga kabla ya kuanza masomo ya asubuhi.

Shughuli za masomo zilisitishwa jana katika shule hiyo ya hadhi ya kitaifa, wanafunzi hao wenye ghadhabu walipozua fujo zilizoanza Jumatatu usiku.

Kisa hicho cha ubakaji kilifanyika umbali wa mita 20 kutoka eneo ambako kuna nyumba wanakoishi walimu.

Wanafunzi hao 306 wa Kidato cha Nne walitembea umbali wa kilomita sita kutoka Lugulu hadi kituo cha polisi cha Webuye wakishinikiza mshukiwa akamatwe. Walidai mbakaji huyo analindwa na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Bi Dinaa Cheruiyot.

Huku wakiwa wamebabe mabango na wakiimba nyimbo za kulaani kitendo hicho, wanafunzi hao walitaka mwenzao atendewe haki.

Walidai mwenzao alirauka mapema kama kawaida na kuelekea katika bafu kuoga kabla ya mwanamume ambaye hakutambuliwa, na aliyekuwa uchi wa mnyama, kutokea ghafla na kumbaka.

Aliokolewa na wenzake waliokuwa katika bafu nyingine ambao walipiga mayowe kabla ya jamaa huyo kutoroka na kupotea gizani.

Mwathiriwa alikimbizwa katika zahanati la shule ambako wauguzi walimpa huduma ya kwanza.

Wanafunzi walishangaa ni jinsi gani mwanamume huyo aliingia ndani ya shule ambayo imezingirwa na ua.

Wakiongea na wanahabari katika kituo cha polisi cha Webuye, wanafunzi hao walisema walikasirishwa na matamshi ya mwalimu wao mkuu baada ya tukio hilo.

Mwanafunzi huyo vile vile aliwasuta baadhi ya walimu na wafanyakazi wa shule hiyo kwa kuwanyanyasa kimapenzi kutokana na uchache wao kutokana na janga la Covid-19.

Afisa wa ubora wa elimu katika kaunti ya Bungoma, Caleb Omondi aliwasihi wanafunzi hao kurejea shule akiahidi kulishughulikia suala hilo.