Habari

'Wanafunzi waliojaribu kumtapeli Jakoyo Midiwo Sh100,000 walitumia simu ya Sabina Chege'

March 14th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WANAFUNZI wawili wa Chuo Kikuu cha MultiMedia (MMU) walishtakiwa Jumatano kwa kujaribu kumtapeli mbunge wa zamani wa Gem, Bw Jakoyo Midiwo Sh100,000 wakijifanya wametumwa na Mbunge Mwanamke wa kaunti ya Murang’a, Bi Sabina Chege.

Wanafunzi hao, Derick Kimutai Ng’etich na Edwin Ndiritu Warukira, walishtakiwa mbele ya Hakimu Mkuu, Francis Andayi.

Ng’etich na Warukira walikana walijaribu kumtapeli Bw Midiwo Sh100,000 wakidai wametumwa na Mwakilishi Mwanamke wa kaunti ya Murang’a, Bi Sabina Chege.

Mahakama iliambiwa wanafunzi hao walikuwa wanamtumia Bw Midiwo jumbe wakitumia nambari ya simu ya Bi Chege.

Kwa mujibu wa ujumbe uliomfikia Bw Midiwo, Bi Chege alikuwa anahitaji Sh20,000 ajisaidie kwa vile akaunti yake ya benki ilikuwa imefungwa na alikuwa anasafiri kutoka Mombasa hadi Nairobi na angemrudishia akirekebisha masuala katika benki yake.

Na wakati huo huo msaidizi  wa mbunge mbishi na mwenye siasa kali  wa Suba Kaskazini, Millie Odhiambo alishtakiwa kwa kumtusi katika mtandao mbunge wa Rangwe akidai “ni mwizi na hafai kuwa mwakilishi wa eneo la Rangwe.”

Bw Derick Ochieng Ogayo msaidizi wa Bi Odhiambo alikana alimtusi Bi Gogo na kumweleza hakimu mkuu Francis Andayi “shtaka hili linalenga kuniangamiza kikazi.”

Akasema: “Mimi ni mwanahabari. Nimeoa . Tumejaliwa watoto watatu wanaonitegemea pamoja na mama yao. Naomba uniachilie kwa dhamana. Sikuchapisha maneno mabaya katika mtandao wa Facebook wa Bi Gogo. Nimesalitiwa kabisa.”

Andayi aliwaachilia wanafunzi hao kwa dhamana ya Sh30,000 pesa tasilimu naye Bw Ogayo akapewa dhamana ya Sh50,000.

Kesi zitasikizwa Aprili 11, 2018.