Wanafunzi 170,000 waliokosa kurejea shuleni wasakwa

Wanafunzi 170,000 waliokosa kurejea shuleni wasakwa

Na LEONARD ONYANGO

TAKRIBANI wanafunzi 170,000 hawajarejea shuleni tangu shule zilipofunguliwa wiki mbili zilizopita licha ya serikali kuagiza machifu kuwasaka.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo umebaini kuwa wengi wa wanafunzi ambao hawajarejea shuleni wameolewa, wamejiingiza katika dawa za kulevya au wanashiriki shughuli za kuwaletea mapato.

Jana, waziri wa Elimu George Magoha alikiri kuwa baadhi ya wanafunzi ambao hawajarejea shuleni wana umri wa zaidi ya miaka 18 hivyo ni vigumu kuwalazimisha kuendelea na masomo yao.

Kwa mfano, katika shule ya Upili ya Wasichana ya Our Lady of Fatima iliyoko mtaani Kariobangi Kaskazini, Nairobi, wanafunzi 24 kati ya 900 hawajarejea.

Kulingana na waziri wa Elimu George Magoha, wanafunzi watano kati ya 24 ambao hawajarejea ni wajawazito na wanakaribia kujifungua.Prof Magoha aliyekuwa akizungumza katika ya Shule ya Wasichana ya Our Lady of Fatima, alisema kuwa idadi kubwa ya wanafunzi katika maeneo kame, ikiwemo Kaunti ya Turkana, hawajarejea shuleni kutokana na ukosefu wa chakula shuleni.

“Malori ya kusafirisha chakula katika maeneo hayo yamekumbwa na changamoto za usafiri njiani kutokana na barabara mbovu. Mwishoni mwa wiki hii shule hizo zitapokea chakula,” akasema Prof Magoha.

Alisema tangu shule kufunguliwa Januari 4, mwaka huu, asilimia 99 ya wanafunzi wamerejea shuleni.“Machifu na maafisa wengine wa serikali wanaendelea kusaka wanafunzi ambao hawajarejea shuleni,” akasema Prof Magoha.

Takwimu za wizara ya Elimu zinaonyesha kuwa takribani watoto milioni 17 wanasoma katika shule za msingi na sekondari humu nchini. Hiyo inamaanisha kuwa wanafunzi 170,000 ambao ni sawa na asilimia moja, hawajulikani waliko.

Wakati huo huo, Waziri Magoha alionya wakuu wa shule dhidi ya kuwafukuza wanafunzi wanaoshindwa kulipa karo.Aliwataka wakuu wa shule kutembelea familia za wanafunzi hao ili kuthibitisha ikiwa zina uwezo wa kulipa karo au la.

“Mna miguu na afya njema. Ni nini kinawazuia kutembelea familia za wanafunzi wanaoshindwa kulipa karo? Ni makosa kumrudisha nyumbani mwanafunzi ambaye familia yake inaishi maisha ya umaskini; hata ukiwafukuza pesa hazitaanguka kutoka mbinguni,” akasema Prof Magoha.

Agizo hilo la wizara ya Elimu limewaweka wakuu wa shule katika njiapanda kwani itakuwa vigumu kwao kutembelea familia za mamia ya wanafunzi wanaoshindwa kulipa karo.

Prof Magoha alipiga marufuku vieuzi au sanitaiza shuleni akisema kuwa huenda vikatumiwa na wanafunzi kuteketeza shule.

“Walimu wahakikishe kuwa hakuna mwanafunzi anayeenda na sanitaiza darasani au katika bweni. Wanaokuja nazo wanyang’anywe kisha wapewe wakati wa kuondoka shuleni. Hii ni kwa sababu tumeanza kushuhudia visa vya shule kuteketezwa kwa kutumia sanitaiza,” akasema.

Prof Magoha alisema kuwa wanafunzi wa Gredi 1 hadi Gredi 3 wanaosomea mitaa ya mabanda na maeneo yenye kiwango kikubwa cha umaskini watapewa uji wa bure na serikali.

Kulingana na Prof Magoha, uji huo ulio na soya, utasaidia ubongo wa watoto kukua vyema.Alisema shule zote za umma za jijini Nairobi zimepokea madawati kutoka kwa serikali.

Shule za Kaunti ya Uasin Gishu zimepokea asilimia 94.7 ya madawati ikifuatiwa na Siaya (asilimia 91.5), Vihiga (asilimia 90), Kisumu (asilimia 88.2), Nyandarua (asilimia 84.5), Nyeri (asilimia 82.8), Kiambu (asilimia 82.4), Migori (asilimia 82.2), Machakos (asilimia 81.9), Murang’a (asilimia 81.8) na Busia (asilimia 81.6).

You can share this post!

ODM wajuta kuingia katika handisheki bila utaratibu

Toyota Kenya kutuza mwanafunzi bora Sh500,000 katika...