Habari Mseto

Wanafunzi wana kiu ya kuelewa mimba, hedhi na magonjwa ya zinaa – Utafiti

June 11th, 2019 1 min read

Na LEONARD ONYANGO

IDADI kubwa ya vijana wanataka elimu kuhusu afya ya uzazi kufundishwa shuleni na vyuoni.

Utafiti uliofanywa na kampuni ya Geopoll, unaonyesha kuwa asilimia 62 ya vijana wana hamu ya kufundishwa shuleni masuala kuhusu hedhi, namna ya kuzuia mimba za mapema na jinsi ya kujikinga na maradhi ya zinaa.

Kulingana na utafiti huo uliofadhiliwa na shirika la JIACTIVATE, asilimia 62 ya wasichana hujifunza kuhusu hedhi kutoka kwa wenzao shuleni na ni asilimia 12 pekee ambao hufunzwa na wazazi.

“Asilimia 38 ya vijana waliohojiwa walisema kuwa wangependa kufundishwa kwa kina kuhusu maambukizi ya virusi vya HIV. Asilimia 22 wanataka kufunzwa kuhusu namna ya kujikinga na mimba za mapema,” akasema Mkurugenzi wa Geopoll, Tavian MacKinnon.

Utafiti unaonyesha zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi katika shule za umma hufundishwa kuhusu afya ya uzazi na namna ya kutangamana baina ya wasichana na wavulana.

Asilimia 52 ya wanafunzi wanaosomea katika shule zinazosimamiwa na dini hawafunzwi kuhusu afya ya uzazi, kwa mujibu wa ripoti.

Utafiti huo umefichua kuwa wazazi wamehepa jukumu lao la kuwafunza watoto kuhusu afya ya uzazi na namna ya kujikinga na mimba za mapema pamoja na maradhi ya zinaa.

Utafiti huo ulifanywa katika kaunti sita za Nairobi, Kilifi, Homa Bay, Narok, Nyeri na Wajir miongoni mwa vijana wa kati ya umri wa miaka 18 na 24.

Ni asilimia tano pekee ya wanafunzi ambao hupata habari kuhusu afya ya uzazi kutoka kwa wazazi wao katika Kaunti ya Nairobi na Homa Bay, inasema ripoti hiyo.

Katika Kaunti ya Kilifi asilimia 11 ya wanafunzi hufunzwa na wazazi wao, Narok (asilimia 4), Nyeri (8) na Wajir (9).

“Kuhusu vurugu katika familia, asilimia 78 ya vijana walikubali kwa kauli moja kuwa mwanamke hafai kupigwa. Asilimia 68 walisema kuna haja ya mwanamke kujiondoa katika ndoa ikiwa atapigwa mara kwa mara na mumewe,’” akasema MacKinnon.