Makala

Wanafunzi wanavyokuza mboga jangwani

September 15th, 2019 3 min read

  NA RICHARD MAOSI

Safari yetu mara hii ilitufikisha katika kaunti ya Samburu, ambayo inapatikana kaskazini mwa taifa la Kenya na raia wengi ni wafugaji wa kuhamahama bila makazi ya kudumu.

Kutokana na hali halisi ya mambo si rahisi kuwaona watu wakijishughulisha na kilimo cha mimea isipokuwa mifugo wanaopatikana kwa wingi,hii ni kutokana na hali mbaya ya anga isiyoweza kufanya mimea kukua.

Licha ya changamoto nyingi Taifa Leo Dijitali ilibahatika kujumuika na wanafunzi wa shule ya msingi ya Suguta Consolata wanaotunza mazingira licha ya uhaba wa maji mbali na kukuza matunda katika mazingira magumu ya mawe.

Shule ya Suguta inapatikana katika kipande cha ardhi ekari tano hivi,ambapo usimamizi wa shule ulitenga nusu ekari ili kuwapatia wanafunzi ujuzi wa kupanda,kupalilia na kutunza mimea yao muda wa ziada.

Mpangilio mzuri wa mimea iliyojaa afya,matunda ,miti na mchanga wenye rutuba ni baadhi ya mambo yaliyobainisha kuwa hawajavunjika moyo kupigana na ukame uliowakodolea macho tangu enzi za mababu zao.

Kulingana na mwalimu Burton Wefwafwa mwalimu wa somo la zaraa na msimamizi wa mradi wa kutunza mazingira anasema amejizatiti kuwafunzisha wanafunzi wake kutumia malighafi haba ya maji yanayopatikana Samburu.

Alieleza kuwa anatumia huduma za wanafunzi kutekeleza jumla kila kitu shambani wakati wao wa mapumziko, na hii ni njia mojawapo ya kuhakikisha wanatumia wakati wao vyema.

Licha ya wanafunzi wengi kukumbwa na changamoto za mimba ya mapema,jamii kuibiana mifugo na ndoa za lazima ni kasumba inayoendelea kupitwa na wakati.

Mwalimu Wefwafwa anasema wanafunzi kutoka chama cha Environmental Club wamefanikiwa kushawishi shule zinazozunguka Consolata kutalii mazingira yao ya kilimo na kujifunza mengi.

Kutokana na mradi huo unaoshirikisha utunzaji wa mazingira,vibarua watatu wamefanikiwa kupata ujira,hususan wakati ambapo shule huwa zimefungwa,kwani usalama unafaa kudumishwa.

Kwa kuwa wanafunzi wengi hapa wanatoka katika familia za wafugaji,upatikanaji wa mbolea ni jambo rahisi kwani wao hupata mbolea kutoka kwa mifugo wao wa nyumbani bila kugharamia.

Awali shirika la Maralal Caritas kutoka eneo la Maralal,liliwakabidhi wanafunzi tanki inayoweza kuhifadhi lita 10,000 ya maji msimu wa mvua,ili yatumike kiangazi inapokuja.

Licha ya changamoto za maji wanaweza kunyunyizia mimea yao maji kupitia mbinu ya drip irrigation ambapo maji hayawezi kuharibiwa wala kupotea.

Kutokana na matunda aina ya machungwa na passion shule huwalisha wanafunzi kwayo mara mbili kwa wiki kwa wiki 15 mtawalia zinazojaza muhula mzima na wakati mwingine zaidi.

Kwa hivyo wanaweza kuhifadhi hadi 7800 kila wiki ambayo ni takriban 50,000 kila mwezi wakati ambapo mavuno ni mazuri, na endapo makali ya jua hayatakausha mimea yao.

Kwa mfano msimu uliopita shule ya Consolata ilivuna matunda ya kutosha na wala hawakununua bidhaa hii kutoka sokoni

Aidha kwenye mazao ya shamba kama vile sukuma wiki na spinach kwa wiki moja shule inaweza kuvuna hadi kilo 100 ambapo kilo moja huuzwa kwa shilingi 100 na kwa sababu hiyo wakahifadhi hadi 10,000 kila wiki .

Kwa jumla faida wanazopata wakulima wachanga katika shule ya msingi ya Suguta Consolata hutumika kukidhi mahitaji ya kimsingi kama vile kununua vitabu na kugharamia elimu ya wanafunzi wanaotoka katika familia maskini.

Mwalimu Wefwafwa anasema amekuwa akijaribu kuwahimiza wanafunzi kufahamu kuwa ni jukumu lao kushiriki katika uhifadhi wa mazingira kwa faida ya kizazi cha baadae.

“Kwa sababu wengi wao hawana ujuzi wa shambani tunawahimiza kushirikiana katika makundi wakati wao wa mapumziko kutunza mimea yao,”akasema.

Dodi Lowapere mwanafunzi wa darasa la nane anatumai kuwa shule yake itaongeza nafasi ya kufanyia kilimo, ili wanafunzi zaidi waweze kushiriki.

Anasema kulingana na desturi za jamii ya wasamburu wamekuwa wakila nyama na maziwa kila siku lakini kila anapokuja shuleni amekuwa akipata lishe mbadala ya majani na matunda ambayo haijazoeleka sana katika jamii yao.

Anasema mradi wa kukuza mimea pia umewapatia wanafunzi hamasa ya kuzingatia umuhimu wa kutunza mazingira kuanzia hatua ya utunzaji miche ,kupanda na kuvuna.

Anasema licha ya changamoto za maji ugumu umewafundisha kutumia malighafi haba kwa makini ili yaje kuwafaidi na kuwafaidi wenzao.

Akilimali ilipata fursa ya kuzungumza na mtaalam wa mimea kutoka eneo la Posta Lanet naye anasema ukulima katika maeneo kame unahitaji subira ya aina yake.

“Ili kutoa nafasi ya kurejesha virutubishi vilivyokuwa vimepotea ni lazima mkulima kuwa na subira ya hali ya juu,”akasema.

Tabitha ansema kuwa ingawa mboga za majani zinahitaji maji mengi spishi ya spinach inaweza kufanya vyema kwenye maeneo kame.

Aliongezea kuwa mkulima anayelenga soko la nje anaweza kupata hela nzuri,bora arekebishe kiwango cha asidi kwenye mchanga,kunyunyizia mimea yake maji na kutumia mbolea kwa wingi.