Habari Mseto

Wanafunzi wapya 5,000 wajiunga na MKU

May 17th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WANAFUNZI wapya wapatao 5,000 wamejiunga na Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) mjini Thika huku wakihimizwa wawe makini masomoni.

Naibu Chansela wa chuo hicho Profesa Stanley Waudo aliwapokea rasmi na kuwahimiza wajiamini kwa yale yote wanayotekeleza chuoni.

Alisema wanafaa kuelewa sheria zote zilizotungwa chuoni ili waweze kuwa makini wanapoendelea na masomo yao.

“Cha muhimu kwa wanafunzi hao ni kuelewa jinsi chuo kinavyoendeshwa, sheria zake, mwelekeo wake, na maswala mengine muhimu yaliyowekwa pale chuoni,” alisema Prof Waudo.

Alikuwa akizungumza katika chuo hicho mnamo Alhamisi alipowapokea wanafunzi wapatao 5,000 wakiwa miongoni mwao 2,800 waliofadhiliwa na serikali kuendelea na masomo yao katika chuo hicho.

Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) Prof Stanley Waudo akijumuika pamoja na wanafunzi wapya waliojiunga na chuo hicho kwa mara ya kwanza. Picha/ Lawrence Ongaro

Wakati wa hafla hiyo wanafunzi hao walifahamishwa umuhimu wa masomo yao katika chuo hicho, maisha ya kibinafsi ya wanafunzi hao, na jinsi ya kukabiliana na mambo magumu wanapokuwa chuoni.

Waliarifiwa jinsi ya kukabilianana na maisha magumu chuoni ambapo walihimizwa kutafuta ushauri kutoka kwa wahadhiri na kushauriwa kutotekwa nyara na maswala ya mapenzi.

Prof Waudo aliwajulisha ya kwamba chuo hicho kipo tayari kuwapa mawaidha wakati wowote watakapohitaji ili wasije wakakabiliwa na msongo wa mawazo wakiwa masomoni.

Alisema hakuna ubaguzi wowote MKU kwa sababu huwasajili wanafunzi kutoka pembe zote ulimwenguni kwa minajili ya kuleta utangamano miongoni mwa wanafunzi wote bila kujali tabaka, kabila au rangi.

“Mafanikio ya mwanafunzi yeyote ni kujiamini na kusoma kwa bidii bila ‘kuazima’ tabia za wengine kiholela,” alisema Prof Waudo.

Aliwahimiza wanafunzi waweze kujumuika pamoja kwa kubadilishana mawazo kwa lengo la kuelewana zaidi.

Wanafunzi hao walionyesha furaha nyusoni mwao wengi ikiwa ni mara yao ya kwanza kujiunga na chuo kikuu huku wakitangamana kwa uwazi.

Wengi wa wanafunzi waliopata nafaji ya kuhutubia wenzao walisema watafuata maagizo yote waliyopewa kwa kuwa makini na yale yote wanayotekeleza wakiwa chuoni.