Habari Mseto

Wanafunzi wapya wa MKU wapewa mwongozo na mwelekeo

November 3rd, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WANAFUNZI wapya waliojiunga na Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) wamehimizwa kujibidiisha masomoni.

Mnamo Jumanne wanafunzi hao wapya walipitia maelezo mwafaka jinsi wanavyostahili kujiendeleza na kutia fora masomo bila kulegea.

Naibu Chansela wa MKU Prof Stanley Waudo, amewapa hamashisho jinsi wanavyostahili kuendesha mambo yao wakiwa chuoni.

Amesema tangu kisa cha kwanza cha Covid-19 kuthibitishwa nchini Machi 13, 2020, wanafunzi katika kila sehemu walipitia masaibu tele, lakini pia hali ya janga hilo ikileta mabadiliko makubwa katika maswala ya masomo na elimu.

“Masomo sasa yanaendeshwa kupitia mtandao wa Intaneti na kwa hivyo kila mwanafunzi atalazimika kufuata mwelekeo huo. Kwa hivyo ni sharti mjizoeshe na hali hiyo,” amesema Prof Waudo.

Ameyasema hayo katika ukumbi mkuu wa chuo hicho alipokuwa akitoa mwelekeo mpya utakaofuatwa wakati wote watakapokuwa huko chuoni.

Amesema masomo kupitia mtandao ndio utakuwa mtindo wa kisasa na wanafunzi waanze kujizoesha.

Amesema ushirikiano wao na kampuni ya huduma za simu na Intaneti ya Safaricom, umeleta mabadiliko kwa sababu wanalipa ada ndogo kwa kutumia mitambo yao ya kidijitali katika chuo hicho.

“Chuo hiki sasa kinaendelea kutumia mawasiliano ya kidijitali kwenye mtandao jambo ambalo ni mafanikio mkubwa kwetu,” amesema.

Amewahimiza wanafunzi hao kutumia nafasi waliopata kwa weledi na wasikubali kupotoshwa na anasa za dunia.

“Ni vyema kuzamia kwenye masomo na kuafikia malengo yenu halafu mengine yatafuata baadaye,” alifafanua.