Habari Mseto

Wanafunzi watuzwa kwa uandishi wa insha

September 27th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

WANAFUNZI Elizabeth Awoton Chibile kutoka Shule ya Msingi ya Kang’alita, Turkana na Mebo Eileen wa Lugulu Girls, Bungoma ndio mabingwa wa makala ya saba ya Shindano la Uandishi wa Insha za Kiswahili linaloendeshwa mitandaoni kila mwaka na shirika la eKitabu.

Chibile ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nane na mwenzake Mebo walitawala Kitengo cha Kiswahili kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Upili mtawalia.

Mbali na kila mmoja wao kujishindia karo ya Sh50,000 pia walituzwa tarakilishi, mashati-tao, kalamu na vyeti kutoka eKitabu na wadhamini wenza wa shindano hilo lililowaleta zaidi ya washiriki 13,500 mwaka 2019.

Chibile aliwapiku Kelly Wekesa Wanjala (Kitale School, Trans-Nzoia), Nachami Lekiliyo (Lempuranai Primary, Samburu), Rahma Abdullahi (Mnara Junior Academy, Garissa), Mwadzumbi Ngome (Mwanda Primary, Kwale) na Charity Nekesa (St Joseph’s Lumino Primary, Kakamega) ambao walishikilia nafasi ya pili hadi sita mtawalia miongoni mwa wanafunzi wa shule za msingi.

Kwa upande wa shule za upili, Mebo aliwabwaga Jepkogei Diana (Moi Girls Eldoret, Uasin Gishu), Hussein Kengo (Maranda High, Siaya), Elias Mbugi (Munithu Day, Meru), Christine Okisai (St Luke High Kimilili, Bungoma) na Pamella Muhonja (Moi Girls Eldoret).

Kinyume na makala ya awali, mashindano ya mwaka huu yalijumuisha pia kategoria za sanaa ya uchoraji na uandishi wa Insha za Kiingereza na Kifaransa miongoni mwa wanafunzi wote wa shule za msingi na za upili wakiwemo wale wasio na uwezo wa kuona (watumiao breli) au kusikia (wanaotumia Lugha Ishara).

Kwa mujibu wa Will Clurman ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa eKitabu, makala yajayo ya mashindano haya yatajumuisha pia kitengo cha Kijerumani.

Hatua hiyo inachochewa na haja ya kupanua wigo wa ushindani miongoni mwa wanafunzi na kuhimiza zaidi makuzi na maenezi ya lugha mbalimbali za kigeni kupitia mitandao.

Walimu, wapenzi wa lugha na wachapishaji walitumia hafla ya kutolewa kwa tuzo hizo mnamo Jumatano wiki hii kuwahimiza wanafunzi kuthamini usomaji wa lugha mitandaoni kwa imani kwamba ni kiwanda kikuu cha maarifa, ajira na uvumbuzi.

Kutatua matatizo

Katika shindano la mwaka 2019, washiriki walitakiwa wajadili jinsi teknolojia ilivyo na uwezo wa kutatua mengi ya matatizo yanayowakabili wanafunzi shuleni.

“Vijana someni sana kwa sababu upekee wa kitabu ni kwamba siku zote huwa benki inayobeba maarifa na elimu,” alisema mmojawapo wa waamuzi wa shindano la mwaka 2019, Bi Beatrice Kavere katika kauli iliyoungwa na walimu wengi waliosisitiza kwamba uandishi wa Insha ndio msingi wa utunzi wa riwaya, novela, hadithi fupi na hata tamthilia.

“Sisi pia tulianzia mahali fulani. Ushindi wa aina hii ni kiamsha hamu kwa wanafunzi hawa kuanza kutambua ukubwa wa uwezo walionao katika masomo ya lugha. Uwezo wao wa kuandika na kujieleza kifasaha kwa lugha wanazozielewa vyema ni kitu ambacho wanapaswa kuwa nacho bila ya kujali taaluma wanazopania kuzizamia baadaye maishani,” akasema Bi Kavere.