Habari za Kaunti

Wanafunzi wawili waaga dunia kwa ajali ya pikipiki

May 14th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

WANAFUNZI wawili wa sekondari kutoka Kaunti ya Kiambu wameripotiwa kuaga dunia baada ya pikipiki yao kupata ajali Jumapili jioni.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kiambu Bw Michael Muchiri, wawili hao walitambuliwa kama Jane Mugure wa Kidato cha Tatu na Francis Muiruri wa Kidato cha Nne katika Shule ya Upili ya Kanjuku iliyoko eneobunge la Gatundu Kusini.

Alisema kwamba wanafunzi hao walikuwa watatu katika pikipiki hiyo ambapo wawili waliaga dunia huku mmoja akiponea lakini akiachwa na majeraha.

“Mwendeshaji wa pikipiki hiyo, ambaye ni mwanafunzi mwenzao kwa jina Brian Mburu, alishindwa kuidhibiti walipogongwa na pikipiki nyingine katika barabara ya Mang’u-Flyover,” akasema Bw Muchiri.

Bw Muchiri aliongeza pikipiki iliyokuwa na hao watatu baada ya kuyumba, ilielekea kwa mkondo wa gari lililokuwa linaenda kwa kasi na ndipo wakagongwa na kurushwa kwa lami.

“Hapo ndipo Jane aliaga dunia akikimbizwa hospitalini huku naye Francis akiaga dunia alipokuwa akitibiwa katika hospitali ya Thika Level 5,” akasema.

Jane Mugure wa Kidato cha Tatu na Francis Muiruri wa Kidato cha Nne ambao waliaga dunia Jumapili. PICHA | HISANI

Mwendeshaji wa pikipiki hiyo nyingine naye aliponyoka mauti akiwa na majeraha.

Brian alisema ni muujiza wa Mungu kwamba yuko hai kwa kuwa “nilisikia tumegongwa kutoka nyuma, nikajipata kwa mkondo wa gari, nikajaribu kulihepa lakini nikasikia tumegongwa kwa upande wa abiria wangu… nikapoteza fahamu”.

Alisema kwamba alirejelewa na fahamu na akawaona wenzake wamelala kwa lami huku umati wa watu ukikusanyika.

“Francis alikuwa akimwita Mungu wake kwa sauti huku Jane akiwa hali mahututi. Waliofika walikawia kutupeleka hospitalini na hii ilifanya wenzangu wawili kupoteza damu nyingi,” akasema Brian.

Alisema kwamba alikuwa ameomba pikipiki hiyo kutoka kwa jirani ili waende kutembelea marafiki na kisha wakafika katika bwawa la Kariminu kulitalii.

“Nasikitika kuhusika katika ajali hiyo iliyoua wawili hao ambao pia ni mabinamu. Ningekuwa na ufahamu kwamba hali ingeishia majonzi hayo singejitolea kuendesha pikipiki hiyo. Lakini Mungu atanipa amani na pia atulize nyoyo za familia na marafiki wa hawa waliotuacha,” akasema Bw Mburu.