Wanafunzi wengi zaidi kusomea chini ya miti 2021

Wanafunzi wengi zaidi kusomea chini ya miti 2021

Na WAANDISHI WETU

IDADI kubwa ya wanafunzi watakaorudi shuleni wiki ijayo, watalazimika kusoma chini ya miti baada ya serikali kushindwa kupanua madarasa ili kuepusha misongamano inayoweza kueneza virusi vya corona.

Waziri wa Elimu Prof George Magoha, Jumatatu alikiri itakuwa changamoto kuepusha mtagusano wa wanafunzi wakati shule zitakapofunguliwa Jumatatu ijayo, na hivyo itabidi walimu na wasimamizi wa shule wawe wabunifu ikiwemo kuwekea watoto madarasa chini ya miti na viwanjani.

Waziri alisema hayo huku walimu wakuu wakiitaka serikali kutoa fedha kwa shule kabla ya Jumatatu ijayo.Walimu hao wa shule za msingi wakiongozwa na mwenyekiti wao wa kitaifa Nicholas Gathemia, walisema shule nyingi hazipo tayari kwa ufunguzi kutokana na uhaba wa madarasa na vifaa vya kuzingatia kanuni za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

“Wanafunzi wote wakirudi shuleni Jumatatu hawatatoshea katika madarasa yaliyopo,” akasema Bw Gathemia. Bi Phoebe Kittoi wa Shule ya Msingi ya Magadi, alisema wanatarajia idadi ya wanafunzi katika shule za umma kuwa ya juu zaidi kutokana na kufungwa kwa shule nyingi za kibinafsi.

Kufikia sasa shule za kibinafsi 227 za msingi na sekondari zimefungwa kutokana na madhara ya Covid-19, na kuwaacha wanafunzi wapatao 56,000 bila pa kusomea.

Wengi wa wanafunzi hawa watalazimika kujiunga na shule za umma na hivyo kuongeza msongamano.Walimu hao waliokutana Nairobi walisema serikali inapasa kutenga fedha za matibabu ya walimu na wanafunzi ambao huenda wakaambukizwa virusi vya corona shule zikifunguliwa.

Katika hotuba ya kitaifa kuhusu hali ya Covid-19 nchini mnamo Novemba, Rais Uhuru Kenyatta alihimiza wabunge washauriane na bodi za Hazina ya Kitaifa ya Ustawishaji Maeneobunge (NG-CDF) ili kufadhili maandalizi ya shule kabla watoto wote warudi Januari.

Miongoni mwa masuala yaliyohitajika kufadhiliwa ni pamoja na kuweka sehemu za kuosha mikono, usambazaji barakoa, usafi na upanuzi wa madarasa ili kuepusha mtagusano.

MISONGAMANO

Kwa kawaida, shule za umma huwa na msongamano wa wanafunzi madarasani na vile vile katika mabweni.Katika kipindi ambapo wanafunzi wa Darasa la Nne, Darasa la Nane na Kidato cha Nne walikuwa shuleni, baadhi ya shule zilikuwa zikitumia madarasa ya wanafunzi ambao walikuwa wangali nyumbani kuepusha mtagusano.

Kwa msingi huu, changamoto itatokea wakati watoto wote watakaporudi shuleni kuanzia Jumatatu.Serikali ilikuwa imezindua mpango wa kusambazia shule madawati 650,000 lakini imeonekana hapakuwepo mpango mahsusi kuhusu sehemu ambapo madawati hayo yangetumiwa.

Prof Magoha alisema kufikia jana, madawati takriban 500,000 yalikuwa tayari yamesambazwa kwa shule zilizo sehemu mbalimbali za nchi.Kando na ukosefu wa madarasa, serikali jana ilisisitiza haitasambazia wanafunzi wote barakoa isipokuwa milioni tatu pekee ambao wametambuliwa kutoka katika familia zisizojiweza kifedha.

“Wazazi wajue hili ni suala muhimu sana. Familia zinaweza kugharamia barakoa ya Sh100 nzuri ambayo inaweza kuoshwa. Msisubiri barakoa kutoka kwetu. Nendeni mnunulie watoto wenu,” akasema waziri.

Prof Magoha aliongeza kuwa wizara yake inaendelea kushauriana na Wizara ya Fedha ili Sh19 bilioni zinazohitajika shuleni kwa Muhula wa Pili utakaoanza Januari zitolewe haraka.Walimu wakuu wamekuwa wakilalamika hawajapokea fedha ilhali wanahitajika kukamilisha maandalizi ya kufungua shule.

Huku hayo yakijiri, foleni ndefu zilishuhudiwa katika maduka ya vitabu na sare za shule katika miji tofauti.Wamiliki wa maduka hayo walilazimika kuchukua usukani ili kuhakikisha miongozo ya idara ya afya kuhusu umbali inafuatwa kikamilifu.

Wanunuzi walipanga foleni nje ya maduka hayo ambapo idadi chache ya watu iliruhusiwa kuingia ndani kwa zamu na kuzingatia mipangilio maalum.

Maduka mengi ya sare yamekuwa wazi siku zote isipokuwa siku kuu ya Krisimasi ambapo yalifungwa kwa muda.Wamiliki walisema japo wazazi wameanza kumiminika, huenda idadi yao ikaongezeka hata zaidi mwishoni mwa wiki hii na mwezi ujao.

Maduka hayo tayari yamejazwa vifaa mbalimbali vya shule ili kutosheleza mahitaji ya wanunuzi.

Ripoti za Victor Raballa, Faith Nyamai, Valentine Obara na Phyllis Musasia

You can share this post!

Makanisa yaililia serikali kuyaruhusu kuandaa kesha za...

Maseneta mbioni kupitisha marekebisho ya Sheria ya Pufya