Habari Mseto

Wanafunzi wote kunufaika na bima ya afya

January 9th, 2020 2 min read

Na FAITH NYAMAI

WANAFUNZI wote milioni 10 nchini watapokea bima ya serikali ya afya mwaka huu bila kujali iwapo maelezo yao yamejumuishwa katika Mfumo wa Kitaifa wa Kuhifadhi Habari kuhusu Elimu (NEMIS) au la.

Waziri wa Elimu Profesa George Magoha jana alisema walimu wakuu wa shule sasa wanahitajika kuwahesabu wanafunzi wao katika shule za msingi na za upili na kuwasilisha data hiyo kwa Wizara ya Elimu ili kuwezesha usambazaji wa fedha katika taasisi hizo.

“Masuala ya habari za wanafunzi kutoweka katika Nemis kwa sababu hawana cheti cha kuzaliwa hayapaswi kuwa kizingiti dhidi ya haki ya wanafunzi ya kupata elimu,” alisema Bw Magoha.

Waziri huyo alisema serikali itasambaza fedha shuleni ili kuwezesha uendeshwaji shwari wa taasisi hizo katika muhula wa kwanza.

Aidha, alisema watahiniwa wote wa darasa la nane na kidato cha kwanza pia watasajiliwa kwa mitihani yao ya kitaifa mwaka huu pasipo kujali ikiwa wana vyeti vya kuzaliwa au la.

Serikali imekuwa ikisambaza fedha shuleni kuwafadhili wanafunzi ambao habari zao zimejumuishwa katika Nemis.

Wanafunzi wa sekondari pia hawawezi kupata Bima ya Afya Nchini katika mpango wa elimu ikiwa habari zao hazijajumuishwa katika Nemis.

Mfumo huo huwatambulisha wanafunzi kwa kutumia data iliyojumuishwa na kutuma habari hizo kwa NHIF kwa matibabu.

“Changamoto chache ambazo shule zimekumbana nazo wakati wa kujumuisha maelezo ya wanafunzi kwa kutumia Nemis zinasuluhishwa na Wizara,” alisema.

Waziri huyo alikuwa akizungumza jana katika uzinduzi wa Mpango wa Ufadhili kuhusu Elimu.

Ufadhili huo umenufaisha wanafunzi 9,000 maskini kutoka maeneo 110 na miji 15 yenye vitongoji duni.

Mpango huo unafadhiliwa na Mradi wa Kuboresha Viwango vya Ubora katika Elimu ya Sekondari (SEQIP) na Wizara ya Elimu, kwa usaidizi kutoka kwa Benki ya Dunia na unatekelezwa kupitia Wakfu wa Equity Group

Ufadhili huo wa Sh3 bilioni ambao sasa upo katika mwaka wake wa pili umedhamiriwa kuhakikisha kwamba watahiniwa wote wa KCPE 2019 ambao ni maskini na wasiojiweza wanasaidiwa kujiunga na shule walizochagua.