Habari Mseto

'Wanahabari 400 wamepoteza ajira sababu ya corona'

October 31st, 2020 1 min read

Na Justus Ochieng

WANAHABARI zaidi ya 400 wamefutwa kazi tangu janga la corona lilipoingia nchini.Kwa mujibu wa Shirikisho la Wahariri wa Kenya (KEG), wanahabari wengine ambao bado wako kazini walilazimika kukubali kupunguziwa mishahara.

“Wale ambao bado wana kazi wanapokea mishahara iliyopunguzwa kwa kati ya asilimia 10 hadi 30,” akasema Rais wa KEG, Bw Churchill Otieno.

Kulingana naye, hali hii ilisababishwa na kuwa mashirika ya habari pia yaliathirika kiuchumi.Alisema sekta ya habari ni muhimu kukuza demokrasia ya nchi kwa hivyo hali hii inafaa kutia kila mwananchi wasiwasi.

“Kama sekta huru ya habari ni muhimu kwa demokrasia yetu, basi kufilisika kwa mashirika ya habari si suala la wafanyabiashara wa kibinafsi bali litatuathiri sote,” akasema.

Alikuwa akizungumza Nairobi katika hafla iliyoandaliwa na KEG kwa kaulimbiu ya “jukumu la sekta ya habari kutoa mwongozo kwa mdahalo wa Mpango wa Maridhiano (BBI)’.