Habari Mseto

Wanahabari wahamasisha wazazi kuhusu hatari za mimba za mapema

June 12th, 2020 1 min read

NA WAWERU WAIRIMU

KATIKA kipindi hiki cha Covid-19 ambapo wanafunzi wote wako nyumbani, wako katika hatari ya kujipata katika vikundi vya utumiaji wa mihadarati au ndani ya ndoa za mapema ambazo zinaweza kuzima ndoto zao za baadaye.

Huku wazazi waking’ang’ana na hali hii ngumu, hawapati wakati mwafaka wa kuwapa wanao nasaha kwa sababu wajishughulisha kuwatafutia chakula, kodi ya nyumba na gharama zingine

Wasichana kutoka jamii nyingi wako kwenye hatari ya ukeketaji, utamaduni ambao umepigwa marufuku kwa kuhusishwa na kuathiri vibaya afya yao.

Wasichana wengi walio nyumbani, kwa muda wa zaidi ya miezi mitatu sasa,  hawapati vifaa muhimu vya kiafya kama kama sodo amabazo walikuwa wakipewa bure shuleni. Hii, kulingana na wataalamu, inaweza kuwachochea kusaka hela za kununua sodo kupitia ngono kiholela.

Huku wakielewa hatari zinazo wakodolea macho wasichana, kituo kimoja cha redio katika Kaunti ya Isiolo – Radio Shahidi – kimeanzisha hamasisho la kuwafunua macho wazazi kuhusu kuwatunza watoto wao inavyostahili.

“Tunaelewa matatizo wanayopitia wanafunzi wakiwa nyumbani, tunaamini kwamba kampeni hii itasaidia kuhakikisha usalama wao na ulinzi wa haki zao,” alisema mkurugezi wa kituo hicho cha redio Simon Githaiga.

Wakitumia gari lenye maspika, wanahabari wa Radio Shahidi wamekuwa wakitembea mitaani wakieneza umuhimu wa wazazi kujua watoto wao wanatangamana vipi na watu wengine wasije wakaingizwa kwa mambo ya uhuni.

Mradi huo pia unalenga kuangazia unyanyasaji wa nyumbani unaotokana na kafyu.