Habari

Wanahabari wahimizwa waendelee kuanika uozo katika jamii licha ya changamoto

September 4th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WANAHABARI wamehimizwa wajizatiti na kuendesha kazi yao kwa ukakamavu licha ya changamoto zilizopo.

Mwenyekiti mkuu wa chama cha Waandishi wa Mashinani – Kenya Correspondents Association (KCA) – Bw William Oloo Janak amewahimiza waandishi, hasa wa mashinani, wawe mstari wa mbele kuangazia maswala tata na tete yanayoshuhudiwa katika serikali za kaunti kote nchini.

Ameyasema hayo Jumatano katika hoteli moja jijini Nairobi.

Kongamano hilo la siku mbili (Septemba 4-5, 2019) limewaleta pamoja waandishi wapatao 80 kutoka kaunti zote za nchi na washikadau mashuhuri kutoka maeneo tofauti.

Mada kuu katika kongamano hili ni: Vyombo Vya Habari na Changamoto za Kuripoti Ugatuzi yaani kwa Kiingereza ‘Media and Challenges of Reporting Devolution’.

Baadhi ya mashirika yaliyofadhili na kuhakikisha kongamano linafana ni Katiba Institute, Irex, Human Rights Watch, Article 19, Transparency International, National Coalition, Action for Transparency, na DW Akademie.

Wanahabari kutoka nchi tofauti kama Tanzania, Uganda, Sudan, na Rwanda pia wanahudhuria.

Mwakilishi wa shirika la Habari la Kenya (KBC) Bi Rachael Nakitare, amewahimiza waandishi wawe mstari wa mbele kuandika na kuripoti maswala ya ufisadi kikamilifu.

“Kila mara waandishi wanapoangazia ufisadi, wao huacha maswala hayo bila kukamilisha habari hizo hadi mwisho. Ni vyema kufuatilia hadi habari ikamilike,” amesema Bi Nakitare.

Aliwashauri waandishi wawe na uwajibikaji wanapoeleza maswala ya kijamii.

Aliyekuwa Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Nyeri Bi Priscilla Nyokabi, ambaye amekuwa mgeni wa heshima amewahimiza waandishi wa habari wawe katika mstari wa mbele kuangazia maswala tata ya serikali za kaunti.

Amesema waandishi wana haki ya kuangazia maswala muhimu ya raia walioko mashinani pamoja na changamoto zao.

“Maswala muhimu yanayostahili kuandikwa ni ya afya, kilimo, na miundomsingi,” amesema Bi Nyokabi.

Amewashajiisha wanahabari kuwataka viongozi wanaosafiri nchi za nje waeleze mambo mengi wanayokuwa wameyashuhudia huko.

Ametoa wito kwa waandishi wa mashinani watambulike kwa sababu wanatekeleza wajibu muhimu katika maeneo hayo.

Mwakilishi wa Shirika la Irex Bi Dinah Kituyi, amesema waandishi wa habari wanapitia masaibu mengi na wanahitaji ushauri wa kisaikolojia.

“Wengi wao hupitia mambo mazito wakiwa kazini na mara nyingi matukio hayo husababisha msongo wa mawazo,” amesema Bi Kituyi.

Naye Bw Francis Ndegwa wa shirika la kutetea haki za kibinadamu la National Coalition Human Right Protection, amesema shirika hilo liko tayari kutetea waandishi wa habari wakati wowote wanapopitia masaibu mengi.

Bi Sheila Masinde wa shirika la Transparency International, amesema waandishi wana kibarua kikubwa cha kuangazia maswala ya ufisadi ili kuelezea wananchi kinachoendelea nchini.

Alisema ni muhimu kutafuta data sahihi kuhusu ufisadi ili kuandika mambo au taarifa zenye mashiko kwa raia na wafuatiliaji wengine wa habari hizo.

Aidha, wanahabari wamehimizwa kushinikiza asasi za serikali, hasa serikali za kaunti kutoa habari muhimu kuhusu masuala muhimu kama kandarasi, mikakati kuhusu mipango ya afya, kilimo na kadhalika.

Vyombo hivyo vimehimizwa kufichua uozo katika jamii bila kuwaogopa wanasiasa au watu wengine wenye ushawishi katika jamii.