Habari Mseto

Wanahabari wakejeli wahubiri wanaowatishia maisha kwa kuanika maovu yao

March 14th, 2019 2 min read

Na ANITA CHEPKOECH

VYAMA vya waandishi habari nchini vimeelezea wasiwasi wake kuhusu ongezeko la visa vya viongozi wa kidini kuwatishia wanahabari wanaofichua maovu na hadaa ndani ya makanisa yao.

Kupitia taarifa, Muungano wa Sekta ya Vyombo vya Habari (KMSWG) ambao hujumuisha Muungano wa Wanahabari (KUJ) na vyombo vya Habari vya Kenya (MCK), uliwashtumu viongozi wa makanisa wanaowatishia wanahabari kwa lengo la kuwazuia kufanya kazi zao kikamilifu.

Taarifa hiyo inajiri huku mhubiri wa Kanisa la Neno Evangelism, James Ngáng’a alinakiliwa kwenye kanda ya video akimtishia mwanahabari wa runinga ya Citizen, Linus Kaikai, akisema ‘ataona moto’ iwapo hatakoma kuwadharau wahubiri.

Majuzi, wafuasi sugu wa mhubiri anayejidai kwa nabii pekee wa Mungu, Dkt David Owuor walijitosa kwenye mitandao ya kijamii na kuvamia vyombo vya habari na maripota, baada ya kuangazia madai ya kutwaa mali ya muumini yaliyokuwa yakimkabili nabii wao.

“Tumesikitishwa na tabia inayochipuka ya viongozi wa makanisa wenye maadili ya kutiliwa shaka kugeukia vyombo vya habari, kuwatisha wanahabari na kuvuruga uhuru wa kujielezea.”

“Uanahabari ndiyo nguzo ya nne ya utawala nchini na una jukumu ya kuanika mambo yanayokwenda mrama kwa umma, wakiwemo viongozi wa makanisa wanaowahadaa waumini wao. Kazi za wakuu wa dini zina athari katika jamii na lazima ziangaziwe bila uoga wala aibu,” ikasema taarifa ya KMSWG.

Nabii Owuor na Kasisi Ngángá ni baadhi ya viongozi wa kidini ambao wamewachochea waumini wao kuzama mitandaoni sio tu kuwakashifu wanahabari bali pia kuwatishia kwa kuendelea kuwaangazia.

“Tumeshtushwa kuwa Ngángá, mtumishi wa Mungu amewatishia wanahabari kwa kumwaangazia. Tunataka kuwaeleza Bw Ngángá na Bw Owuor kwamba, hata wanahabari wanaamini Mungu na hakuna vitisho vyovyote vitakavyowazuia kuanika maovu yanayoendelea katika maeneo ya kuabudu,” ikaongeza taarifa hiyo.

Wakinukuu kifungu cha Bibilia, viongozi wa KMSWG walisema hata Yesu aliingia hekaluni na kuwacharaza viboko watu waliokuwa wakishiriki maovu ndani ya nyumba ya Mungu.

“Uanahabari si uhalifu na utaendelea kuwa macho yanayoangazia taasisi zote na uongozi wa nchi. Hatuwezi kukaa kitako na kutazama tu jinsi wahubiri wanavyowafilisi kondoo wao kwa kisingizio kwamba hawawezi kukabiliwa kisheria,” ikasisitiza taarifa hiyo.

KMSWG hata hivyo ilizitaka Tume ya Kitaifa ya Huduma ya Polisi(NPS) na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma(DPP) kuwachukulia hatua kali Bw Owuor na Bw Ngáng’a kwa kuwatishia wanahabari na wafuasi wao wanaoendeleza shutuma kwenye mitandao ya kijamii kwa walio na mitazamo tofauti.