Habari Mseto

Wanahabari waliohariri picha za ngono za Echesa kizimbani

October 26th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WANAHABARI watatu Mabw David Ndolo, Stafford Ondego na Alex Njue waliokamatwa Jumatatu kwa makosa ya uhalifu wa mitandao waliachiliwa Ijumaa bila kushtakiwa.

Watatu hao walifikishwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi lakini wakaponyoka bila ya kushtakiwa.

Bw Andayi alifahamishwa na washtakiwa hao kwamba walifunguliwa mashtaka chini ya kifungu cha sheria kilichopigwa marufuku na mahakama kuu.

Mahakama ilifahamishwa kuwa watatu hao walishtakiwa chini ya kifungu cha sheria za uhalifu wa kimitandao kilichopigwa marufuku na mahakama kuu miezi mitatu iliyopita.

“Naomba mahakama ifutilie mbali kesi dhidi yetu kwa vile tumefikishwa kortini chini ya kifungu cha sheria kilichopigwa marufuku,” Bw Ondego alimweleza hakimu.

Washtakiwa hao walikuwa washtakiwe kwa kutumiwa na Waziri wa Michezo Rashid Echesa kumharibia sifa  Seneta wa Kakamega Cleopas Malala.

“Mashtaka dhidi yenu yana kasoro na hii korti imewaachilia,” Bw Andayi aliwaeleza washtakiwa hao.

Hawakujibu mashtaka na kesi dhidi yao ilipigwa kalamu.

Akiwahutubia wanahabari Seneta huyo wa chama cha ANC Jumatano aliwaambia wanhabari katika majengo ya bunge kwamba Bw Echesa, kwa ushirikiano na wanahabari fulani, walisambaza  picha hizo mitandaoni zinazomwosha Bw Malala akila uroda na kimada akiwa uchi wa mnyama.