Habari Mseto

Wanahabari wanaoangazia kesi za bangi kulindwa

November 7th, 2018 1 min read

Na ISABEL GITHAE

MAAFISA wa polisi wa kaunti ya Meru wamewahakishia wanahabari wanaofanya kazi katika eneo hilo usalama wao wanapoangazia kesi ya washukiwa sita wa ulanguzi wa bangi.

Hii ni baada ya wafuasi wa mshukiwa mkuu, James Muthiora, maarufu kama Karinta, kutisha kuwavamia wanahabari wawili waliokuwa wakifuatilia kesi hiyo katika mahakama ya Meru.

“Endeleeni kuandika hiyo stori na kuwapiga picha tutapatana kona mbaya,” akasema mmoja wa wafuasi wake.

“Tunaweza kumaliza saa hii na tusione kama ni kitu. Hili si jambo kubwa kwetu,” akatisha mfuasi mwingine.

Kwa bahati nzuri, Mkuu wa idara ya Upelelezi wa Jinai (DCIO) kaunti ya Meru James Githinji na wakili wa mshukiwa Mugambi Kiogora walikuwepo wakati wa tukio hilo na wakawapa onyo kali wafuasi hao.

Kwa upande wake, OCPD wa Meru Peter Kimani alisema alipashwa habari kuhusu vitisho hivyo na DCIO na akawahakikishia wanahabari ulinzi mkali wanapoangazia kesi hiyo.

“Tutaimarisha usalama na pia kuwatuma maafisa wa ujasusi wanaovalia mavazi ya kawaida kila mara mtakapokuwa mkiangazia kesi hii ili waweze kuwanasa watakaolenga kuwadhuru,” akasema Bw Kimani.

Bw Karinta, mkewe Fridah Karimi Muthiora na washtakiwa wengine Timothy Kinoti, Josephat Ekeno Ekeno, Robin Nyaga na Jacob Mukunyu walikamatwa Alhamisi iliyopita polisi walipovamia makazi ya familia ya Bw Karinta.

Hii ni baada ya maafisa hao kupokea fununu kutoka kwa umma kwamba Bw Karinta, anayesemekana kuwa muuzaji maarufu wa bangi kaunti ya Meru, alikuwa akiwauzia watoto wa shule dawa hiyo ya kulevya.