Wanahabari wapinga kuzuiwa kuingia bunge

Wanahabari wapinga kuzuiwa kuingia bunge

NA CHARLES WASONGA

WANAHABARI wanaoripoti habari za bunge wamepinga kauli za baadhi ya wabunge kwamba wazuiwe kuingia bunge wakisema hiyo ni sawa na kuhujumu uhuru wa wanahabari.

Kwenye taarifa, mwenyekiti wa chama cha wanahabari wa bunge (KPJA) Duncan Khaemba jana Alhamisi alisema kuwa uhuru wa wanahabari unalindwa na Katiba ya sasa na wabunge hawana mamlaka ya kuuondoa.

“Kuzuia wanahabari kuripoti bungeni kwa kutoripoti kila kitu ambacho wabunge husema hakuna maana kwa sababu sio kila kitu wabunge husema ni habari inayofaa kupeperushwa au kuandikwa magazetini. Habari zitakazopeperusha huwa ni zile zinazoendeleza masilahi ya umma, sio masilahi finyu ya wabunge,” akasema Bw Khaemba huku akiongeza kuwa uamuzi kuhusu iwapo taarifa fulani kutoka bunge zinafaa kutumika au la hufanywa na wahariri wala sio wanahabari husika.

Mwenyekiti huyo pia aliwashutumu wabunge waliodai juzi kwamba wanahabari hao huwa hawavalii nadhifu wakiwa bunge.

“Bunge lina kanuni kuhusu mavazi ambayo sharti yazingatiwe na wote wakiwemo wanahabari. Kuna walinzi katika malango yote ya bunge ambao huhakikisha hakuna anayeingia akiwa amevalia visivyo,” akaeleza.

Mnamo Jumatano, wakiwa Mombasa, wabunge Tim Wanyonyi (Westlands), Richard Mbui (Kathiani), Jane Kihara (Naivasha) miongoni mwa wengine waliwasuta wahabari kwa kutoa taarifa za kupotosha kuhusu matukio ya bunge.

“Kwa kuwa wanahabari hao hutoa habari za kupotosha, huenda tukapendekeza kuwa kituo cha wanahabari kiondolewe bungeni kwa sababu hakina maana kwetu,” akasema Bw Wanyonyi.

Naye Mbunge wa Kitui Kusini Rachael Nyamai aliwakashifu wanahabari kwa kile alichotaja kama “mwenendo wao kuvalia mavazi ya aibu wakiwa katika majengo ya bunge”.

“Inaonekana kuna hitilafu kuhusu namna bunge huendesha shughuli zake haswa kuhusiana na mavazi ya watu na kundi kubwa ya wanahabari tulio nao bungeni. Tungependa kufanya mazungumzo na uongozi wa bunge haswa kuhusu jinsi wanahabari wenye umri mdogo huvalia kwani mavazi yao huwa sio ya heshima,” akaelaza.

Bi Nyamai alitetea kauli yake akisema kuwa bunge kama asasi lina watu wenye heshima, wakiwemo wazazi. Lakini hakusema lolote kuhusu kanuni kuhusu mavazi na wajibu wa idara ya ulinzi bungeni katika kuhakikisha kuwa kila anayeingia humo amevalia nadhifu.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Vyombo vya Habari Nchini (MCK) David Omwoyo, ambaye alikuwepo katika mkutano, aliahidi kuwasilisha malalamishi ya wabunge kwa wamiliki wa vyombo vya habari.

Hata hivyo, Bw Omwoyo alielekeza kidole kwa wabunge akisema baadhi yao ni wamiliki wa vyombo vya habari na hukosa kuwalipa wanahabari, hali inayofanya baadhi yao kiuka maadili ya taaluma ya uanahabari.

“Baadhi yetu hapa ni wamiliki wa redio, televisheni na vyombo vingine vya habari. Wengine wenu mlikoma kuwalipa wanahabari baada ya kutamatika kwa uchaguzi mkuu. Bila shaka hali hii ndio imechangia matatizo hayo ambayo mwaangazia hapa leo (Jumatano). Lakini kama MCK tufuatilia masuala hayo na wamiliki wa vyombo hivyo,” akaeleza.

  • Tags

You can share this post!

Natembeya akosoa uongozi wa mtangulizi wake

Real Madrid wazamisha Valencia na kukaribia tena Barcelona...

T L