Habari Mseto

Wanahabari wataka sheria zinazowafyonza pesa zibanduliwe


MUUNGANO wa Wanahabari wa Bunge la Kitaifa Nchini (KPJA) umewasilisha malalamishi kwa Afisi ya Mwanasheria Mkuu, Justin Muturi, ukimtaka aingilie kati kuwezesha sheria kadhaa zinazoathiri vyombo vya habari kufanyiwa marekebisho.

Bw Muturi alipokea nakala ya malalamishi hayo Jumatano katika Afisi ya Sheria Nchini, jijini Nairobi, kutoka kwa kundi la viongozi na wanachama wa Muungano huo wakiwemo Mwenyekiti wa KPJA, Duncan Khaemba na Katibu Mkuu Julius Otieno.

Haya yamejiri wakati ambapo kampuni kadhaa za vyombo vya habari zinakabiliwa na wakati mgumu kuendeleza shughuli zake, huku baadhi zikiwa zimesambaratika, baada ya kuzabwa faini ya mabilioni katika kesi hali ambayo imeathiri pakubwa wanahabari na sekta ya habari kwa jumla.

Nakala hiyo imetaja vipengee kadhaa ikiwemo Kipengee 411A cha Sheria kuhusu Habari na Mawasiliano Nchini na Kipengee 63 cha Katiba, ambavyo Mahakama Kuu tayari imetangaza kwamba havina msingi kikatiba katika kesi kadhaa, ilhali vinaendelea kutumika kuadhibu vyombo vya habari.

“Maamuzi haya hasa yanahusu vyombo vya habari ba wanahabari kwa sababu ni kiini cha haki na uhuru ambao ni muhimu kwa utekelezaji wa Vifungu 33 na 34 vya Katiba ya Kenya 2010 kuhusu Uhuru wa Kujieleza na Uhuru wa Vyombo vya Habari mtawalia,” ilisema nakala hiyo.

Vipengele vinavyokiuka Katiba ya Kenya

Vipengee vinginevyo ambavyo Mahakama Kuu imesema vinakiuka katiba ni pamoja na Kipengee 29 cha Sheria kuhusu Habari na Mawasiliano Nchini, kilichotangaza kuwa hatia “matamshi ya kuchukiza mno” na kauli za uongo zinazoudhi, zinakera au kusababisha taharuki kiholela.

Kipengee 194 cha Katiba kilichounda hatia ya kuchafua jina pamoja na Kipengee 77(1) na (3) cha Katiba kilichobuni hatia ya kudunisha mamlaka ya taasisi au mfumo rasmi.

“Katika hali hii, tunategemea vipengee vya Kifungu 8 cha Tathmini ya Sheria (nambari 1) na Vifungu 5 na 6 vya Sheria kuhusu  Mwanasheria Mkuu (2012) kuomba kwa unyenyekevu ufanyie marekebisho na uondoe kutoka kwenye orodha ya kila mwaka ya Sheria za Kenya ikiwa vifungu hivyo bado vinaandaliwa au kutoka orodha ijayo kulingana na hali ilivyo, kuhusu vipengee vilivyotangazwa kukosa msingi.”

Muungano huo vilevile umeelezea wasiwasi wake kuhusu baadhi ya vifungu vya Sheria kuhusu Matumizi Mabaya ya Tarakilishi na Hatia Kidijitali (Nambari 5 ya 2018) ukihoji kuwa, vinakiuka moja kwa moja Vifungu 33 na 34 na hivi punde korti zitahitajika kurekebisha hali hiyo.

Vinajumuisha Kipengee 22 kinachobuni Hatia ya kuchapisha Uongo, Kipengee 23 kinachobuni Hatia ya Kuchapisha Habari za Uongo na Kipengee 27 kinachobuni Hatia ya Kuhangaisha Kidijitali.

Huku akiahidi kutathmini wasilisho hilo, Mwanasheria Mkuu sheria kadhaa zinazotumika kwa sasa zinahitaji kuangaziwa upya hasa ikizingatiwa kuwa baadhi hazijafanyiwa marekebisho tangu zilipobuniwa zaidi ya mwongo mmoja uliopita licha ya hali kubadilika nchini.