Wanaharakati kortini kupinga Hazina ya Hasla, wataka isitishwe

Wanaharakati kortini kupinga Hazina ya Hasla, wataka isitishwe

NA RICHARD MUNGUTI

MASHIRIKA mawili ya kutetea haki na usimamizi bora wa mali ya umma yamewasilisha kesi kuhoji zinakotoka Sh100 bilioni za Hazina ya Hasla ikitiliwa maanani Bunge halijaidhinisha Hazina Kuu ya Kitaifa kutoa fedha hizo.

Mashirika hayo pamoja na wakili Bernard Odero Okello, yanaomba Mahakama Kuu ipige breki utoaji wa fedha hizi kwa mahasla wakihofu huenda mabilioni haya yakafujwa.

Hazina hii ya mahasla, ilibuniwa na Rais William Ruto mnamo Novemba 30, 2022 hata kabla ya kuteuliwa kwa afisa mkuu wa kuidhibiti na bunge kutenga matumizi ya fedha hizi kutoka Hazina Kuu.Rais Ruto alitangaza pesa hizi zitatolewa katika mfuko wa hazina kuu ya kitaifa.

Katika kesi iliyowasilishwa na wakili Bernard Odero Okello, vyama vya Operation Linda Ugatuzi (OLU) na Integrated Development Network (IDN), mahakama kuu imeelezwa hazina hiyo ilizinduliwa bila kuzingatia sheria za usimamizi wa fedha za umma.

“Bila kuwepo afisa mkuu na bodi iliyoteuliwa ambayo wanachama wake wako na ukwasi mkuu wa masuala ya usimamizi wa pesa za umma na pia sheria kubuniwa kudhibiti hazina hii, basi pesa za umma zitapotea,” asema Okello.

“Rais Ruto alitangaza awamu ya pili ya pesa za kufadhili biashara za mahasla zitatolewa,” kiongozi wa OLU, Prof Fred Ogola alidokeza.

Hivyo basi Bw Okello, Prof Ogola (OLU) na Dennis Wendo wa IDN wameeleza wasiwasi wao wakisema “zaidi ya Sh100bilioni zitatolewa katika hazina kuu kama hakuna sheria za kuzidhibiti.”

Walalamishi walisema: “Tunaomba Mahakama Kuu isitishe utoaji wa fedha hizi za mahasla kwa vile bunge halijazitenga na huenda pesa za umma zikapotea ovyo ovyo.”

Mahakama Kuu iliambiwa bunge la kitaifa halijatenga fedha hizo za hazina ya mahasla kwa mujibu wa sheria nambari 4,5 na 6 kuhusu matumizi ya fedha za umma.

“Hakujabuniwa bodi ya kusimamia fedha hizi za mahasla kwa mujibu wa sheria nambari 10 zilizotungwa na Waziri wa Fedha,” asema wakili Odero.

Hazina hiyo ya Mahasla ilizinduliwa na Rais Dkt William Ruto na kufikia sasa mikopo inayozidi Sh3.69 bilioni imetolewa kwa mahasla.

Prof Ogola (kiongozi wa OLU) na Wendo (kinara wa IDN) waliowasilisha kesi hiyo walisema pesa za umma zinatumiwa vibaya kwa vile hakuna sheria za ukopeshanaji zilizochapishwa katika Gazeti rasmi la Serikali.

“Rais Ruto hajaeleza anakotoa pesa hizi zinazokopeshwa wafanyabiashara wadogo wadogo kuanzia Sh500 kwenda juu,” alisema Prof Ogola anasema katika kesi aliyowasilisha mahakamani.

Msomi huyu aliyebobea katika masuala ya usimamizi wa pesa za umma na maadili bora alisema huenda hazina hii ya Mahasla ikatumika kupora wananchi pesa.

Pia alisema huenda wanaofadhili hazina hii ya Mahasla ni walanguzi wanaotumia hazina hii ya mahasla “kusafisha pesa zilizopatikana kwa njia ya uhalifu.”

Prof Ogola alihoji kiini cha kuwataka wananchi wafichue nambari za mamlaka ya kulipia ushuru (KRA) za kulipia ushuru.

“Uchunguzi tuliofanya umefichua kampuni moja ijulikanayo kwa jina la Finetech ndiyo inayotoa pesa hizi za kufadhili hazina hii ya mahasla. Hatujui iko nchi ipi ulimwenguni,” Prof Ogola alisema.

Mlalamishi huyu anasema katika kesi hiyo hapingi hazina hii ila anaomba mahakama kuu iamuru sheria na vipengee vya sheria za fedha vitungwe kama zile sheria za Uwezo zilivyo.

Kulingana na sheria nambari 24(4) za usimamizi wa pesa za umma, Waziri wa Hazina anatakiwa kutunga sheria za kudhibiti hazina zote.

Kuhusu hazina ya Mahasla,Prof Ogola amesema pesa zimetolewa kutoka mfuko wa hazina kuu bila bodi ya kuzidhibiti.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yafungua kituo kudhibiti uvamizi wa nzige

Kidero agonga mwamba

T L