Habari Mseto

Wanaharakati wa mazingira waitaka serikali iwasaidie waathiriwa wa mafuriko nchini

November 12th, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

WANAHARAKATI wa mazingira wameitaka serikali kufanya upesi kuwasaidia waathiriwa wa mafuriko katika sehemu mbalimbali nchini.

Hii inajiri kabla ya maandalizi ya maandamano ya ‘School Friday for the Climate’ yanayojulikana pia kama ‘Fridays For Future (FFF)’ ambayo hufanyika mara nyingi mwishoni mwa Novemba ambapo mwaka 2019 yataandaliwa tarehe 29.

Fridays for Future ni vuguvugu la kimataifa ambalo hujumuisha wanafunzi ambao huchukua muda kando na masomo yao kufanya maandamano kudai haki katika viti dhidi ya ongezeko la joto duniani.

Wanaharakati hao wanalaumu matumizi ya mafuta yenye madhara kwa mazingira kama njia mojawapo ambayo imechangia katika mafuriko.

“Tumeshuhudia madhara mbalimbali ikiwemo kiangazi na mafuriko. Uharibifu wa mazingira na ukataji miti umechangia katika madhara hayo,” akasema mwanaharakati katika shirika la Greenpeace Africa Bw Amos Wemanya.

Amehimiza serikali kufanya upesi katika kuzuia madhara zaidi katika mazingira.

“Bara zima la Afrika lina jukumu la kuchukua hatua dhidi ya uchafuzi wa mazingira ili kuzuia majanga zaidi,” akasema Bw Wemanya.

Kwa muda wa miezi miwili iliyopita, mvua kubwa imeshuhudiwa katika sehemu mbalimbali nchini ambayo imewaacha watu wengi bila makao.