Habari

Wanaharakati wakamatwa kwa kupinga mradi wa makaa ya mawe

May 26th, 2018 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

WANAHARAKATI wawili wa kutetea haki za kijamii katika kaunti ya Lamu Ijumaa walikamatwa na maafisa wa usalama wakati wakiongoza maandamano ya kupinga kuendelezwa kwa mradi wa nishati ya makaa ya mawe eneo hilo.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Save Lamu ambao hutetea maslahi ya kimazingira na afya ya wakazi eneo hilo, Walid Ahmed Ali, na Mwanachama wa Muungano huo, Is’haq Abubakar Khatib, walijipata pabaya pale polisi ambao hawakuwa wamevalia sare walipojitokeza na kuwakamata ghafla.

Aidha vurugu kati ya maafisa wa polisi na mamia ya waandamanaji ilizuka kabla ya polisi kuwashinda nguvu waandamanaji na kuwachukua wawili hao ambao hadi ripoti hii ikichapishwa walikuwa wakizuiliwa katika kituo cha polisi cha kisiwa cha Lamu.

Wanaharakati wawili wa kijamii, Walid Ahmed (kushoto) na Ish’aq Abubakar Khatib (pili kutoka kulia) wakisindikizwa kituoni na polisi baada ya kukamatwa wakiongoza mamia ya wakazi katika maandamano ya kupinga mradi wa nishati ya makaa ya mawe mjini Lamu Ijumaa Mei 25, 2018. Picha/ Kalume Kazungu

Akithibitisha tukio hilo, Afisa Mkuu wa Polisi (OCPD) wa Lamu Magharibi, Juma Londo, alisema waliwakamata wawili hao baada ya kuongoza maandamano bila idhini.

“Tumewakamata wanachama wawili wa muungano wa kijamii wa Save Lamu. Walikuwa wakiongoza maandamano na mikutano bila idhini kutoka kwa idara ya usalama. Tunawazuilia kituoni kwa mahojiano,” akasema Bw Londo.

Kukamatwa kwa wawili hao kumekashifiwa vikali na wanachama wa mashirika mbalimbali ya kijamii eneo hilo wanaodai serikali inawalenga na kuwakandamiza haki zao wananchi wa Lamu ambao wanapinga kuanzishwa kwa mradi wa nishati ya makaa ya mawe eneo hilo.

Mwenyekiti wa Muungano wa Lamu Marine Forum, Mohamed Athman, alisema kamwe hawatachoka wala kutishwa na serikali katika harakati zao za kuupinga mradi wa nishati ya makaa ya mawe.

Ish’aq Abubakar Khatib ajitupa chini akipinga kukamatwa. Picha/ Kalume Kazungu

Bw Athman alisema mradi huo ni sumu kwa mazingira na afya ya binadamu na hata viumbe wa baharini.

“Wameanza kutukamata wakidhani tutatishika ili kusitisha kampeni zetu za kuupinga mradi wa nishati ya makaa ya mawe. Wakazi wengi hapa Lamu hawana haja na nishati ya makaa ya mawe. Serikali inatulazimisha kuukubali mradi lakini haitafaulu. Tutaendelea kushinikiza kutupiliwa mbali kwa mradi huo wapende wasipende,” akasema Bw Athman.

Mradi huo unaokadiriwa kugharimu kima cha Sh 200 bilioni uko chini ya ufadhili wa Kampuni ya Amu Power.

Jumla ya ekari 975 za ardhi tayari zimetengwa eneo la Kwasasi, tarafa ya Hindi ili kufanikisha ujenzi wa mradi huo unaotarajiwa kuzalisha megawati 1,050 za umeme punde utakapokamilika.