Makala

Wanaharakati wakunja mkia Lamu, kulikoni?

May 31st, 2024 5 min read

NA KALUME KAZUNGU

SHUGHULI za uanaharakati kaunti ya Lamu zinaendelea kudidimia miaka ya hivi karibuni, hali inayoiacha jamii kuhofia dhuluma kuendelezwa eneo hilo bila ‘watetezi’.

Kaunti ya Lamu tayari imesheheni dhuluma za kihistoria, ikiwemo suala la ukosefu wa umiliki wa ardhi miongoni mwa jamii za eneo hilo, ubaguzi wa uwakilishi na ajira serikalini, kutelekezwa kwa jamii katika masuala ya maamuzi ya miradi inayonuiwa Lamu, ukosefu wa maendeleo na kutokuwepo kwa usawa katika ugavi wa rasilimali.

Sababu hizo na nyingine nyingi ndizo zilizochochea Lamu kuamka kiuanaharakati, hasa miaka kati ya 2000 na 2020.

Kwa mfano, katika kisiwa cha Lamu, wiki au mwezi haungepita bila kushuhudia maandamano kadhaa barabarani yaliyoongozwa na wanaharakati, iwe ni katika kuikemea serikali kuu kutoanzisha miradi yenye sumu kwa jamii au kutohusishwa kwa jamii ya Lamu kimaamuzi kuhusiana na miradi mikuu iliyonuiwa kuanzishwa eneo hilo.

Ujio wa miradi mikuu kama vile Bandari ya Lamu (Lapsset), ambayo ilitambulika wazi ingeathiri jamii na hata mazingira kwa kiwango kimoja au kingine pia ilishuhudia pingamizi nyingi kutoka kwa wanaharakati wa Lamu.

Ni kupitia wanaharakati ambapo serikali kuu kupitia Mamlaka ya Bandari nchini (KPA) mnamo Mei,2018 iliamrishwa na Mahakama Kuu ya Malindi kuwafidia wavuvi wapatao 4,734 wa Lamu kitita cha Sh1.76 bilioni.

Maamuzi hayo yanatokana na kubainika kuwa mradi wa Lapsset ulioathiri shughuli za kijamii, ikiwemo uvuvi na masuala mengine ya kimsingi.

Fedha hizo bado hazijatolewa, japo ziko kwenye awamu ya mwishomwisho kabla ya wanufaika kuzipokea.

Ni kutokana na shinikizo za wanaharakati wa Lamu, ambapo wakulima wa maeneo ya Kililana na Mashunduani ambao ardhi zao zilitwaliwa kwa ujenzi wa bandari ya Lamu pia waliweza kufidiwa kima cha Sh1.3 bilioni na serikali kuu mnamo Februari 2015.

Isitoshe, juhudi za wanaharakati wa Lamu zilipelekea kusitishwa kwa mradi wa Sh200 bilioni wa nishati ya makaa ya mawe ulionuiwa kujengwa eneo la Kwasasi, Lamu Magharibi.

Wanaharakati walihoji kuwa mradi huo ni sumu kwa maisha ya jamii na mazingira na kwamba haufai kuendelezwa Lamu.

Jopokazi la Mahakama ya Mazingira (NET) mnamo Juni 2019 lilizingatia pingamizi au shinikizo za wanaharakati hao wa Lamu, hivyo kuafikia kuusitisha mradi huo wa nishati ya makaa ya mawe wa Lamu ambao ulikadiriwa kwamba ungezalisha megawati 1,050 za umeme endapo ungetekelezwa eneo hilo.

Licha ya wanaharakati wa Lamu kujitahidi na hata kuandikisha rekodi hizo za kufaulu katika kampeni zao, miaka ya hivi punde imeshuhudia wengi wa wanaharakati hao hao wakikunja mkia, hivyo kuirejesha Lamu katika enzi za ubaridi, ambapo dhuluma zilikuwa zikiendelezwa huku zikikosa kabisa wa kujitolea kuzikemea.

Je, kulikoni?

Taifa Leo ilifanya uchunguzi wa sababu halisi zinazoyumbisha uanaharakati wa Lamu.

Katika mahojiano na Taifa Leo mnamo Alhamisi, mwanaharakati mkongwe wa Lamu, Bw Mohamed Mbwana Shee alitaja kufariki kwa wanaharakati ngangari na tajika wa Lamu kama vile Abubakar Mohamed Al-Amudy, Abubakar Khatib, Mwalimu Badi, Prof Ali Shekue na wengineo kuwa miongoni mwa vigezo vinavyofisha uanaharakati eneo hilo.

Al-Amudy alifariki mnamo 2020, akiwa na umri wa miaka 70.

Hadi kifo chake, Al-Amudy alikuwa ndiye mzinduzi na mwenyekiti wa muungano wa harakati za kijamii zinazofungamana na ardhi na mazingira wa Save Lamu.

Bw Mbwana anasema licha ya kwamba yeye mwenyewe bado ni mwanaharakati, japo mkongwe, anashikilia kuwa ataendelea na kusalia kuwa mwanaharakati hadi kifo.

Ila anakubali kwamba uanaharakati wa Lamu leo hauna nguvu kama zamani.

“Mimi ni mmojawapo wa waanzilishi wa shughuli za uanaharakati eneo hili miaka ya 2000. Nilipata msukumo zaidi niliposhikana na wazee wenzangu ambao kwa sasa wametangulia mbele za haki, akiwemo Al-Amudy katika kuzisukuma harakati za wanaharakati. Hawa wenzangu walioaga dunia walikuwa mfano mwema kwa Lamu. Kufariki kwao ni pigo kubwa kwa ulimwengu wa uanaharakati Lamu. Na ndio sababu harakati zimefifia,” asema Bw Mbwana.

Mzee Mohamed Mbwana Shee ambaye ni mwanahistoria wa Lamu. Anasema mji wa Mkokoni ulipata jina kutokana na kuwa na ukwasi wa misitu mingi ya mikoko. PICHA | KALUME KAZUNGU

Pia anataja umri, hasa ule wa uzeeni kama yeye kuwa miongoni mwa vizingiti vinavyokosesha uanaharakati joto.

“Baadhi ya wanaharakati kama mimi wamezeeka, hivyo tunakosa siha ya kuendeleza uanaharakati unaohitaji nguvu au zahama kuutekeleza. Ila hatufi moyo,” aongezea.

Bi Raya Famau, mmojawapo wa wanaharakati tajika wa jinsia ya kike Lamu, anasema wanaharakati wengi eneo hilo wamevunjika moyo kutokana na kukosekana kwa mageuzi wa yale wanayopigania na hata kuhatarisha maisha yao.

Bi Famau pia anataja siasa, ambapo wengi wa wanaharakati eneo hilo wamejitosa kwenye ulingo huo, iwe ni katika kutafuta uongozi au kuwaunga mkono wanasiasa fulani ambao tayari matendo yao yafaa kukemewa na wanaharakati.

“Wanaharakati wengi eneo hili wamejitosa siasani na kuwa vibaraka au wafuasi wa viongozi wanaoendeleza maovu au dhuluma katika jamii. Hili limeondoa kabisa ladha ya uanaharakati na kuulemaza. Utawapata hawa wanaharakati wakisukuma hadi kupewa ajira kwenye serikali au utawala wa wanasiasa husika, hivyo kukosa sauti ya kukemea maovu serikalini au uongozini,” asema Bi Famau.

Bi Famau kwa sasa ndiye Afisa Mtendaji wa Shirika la Wanawake wa Lamu, yaani Lamu Women Alliance (LAWA).

Anasema sababu za kufifia kwa uanaharakati Lamu zinatokana na kwamba hata wale wanaojidai kuwa wanaharakati hufanya hivyo kwa maslahi au matumbo yao binafsi na wala si utetezi wa kweli kwa jamii yao.

“Ifahamike kuwa uanaharakati wa kweli ni kazi ya kujitolea mhanga, kumaanisha usitarajie malipo au mshahara wowote. Yaani uanaharakati ni sawa na kuifanya kazi ya kanisa. Usitarajie kwamba utaleta chakula kwa meza kama mwanaharakati. Na ndiyo sababu wengi wakatupilia mbali uanaharakati njiani na kufuata ajira liwe liwalo,” asema.

Naye Bw Ali Athman, ambaye ni mmojawapo wa wazee wa kisiwa cha Lamu, anataja ukosefu wa kujitolea miongoni mwa vijana wa kizazi cha leo kuwa ni miongoni mwa sababu zinazoua uanaharakati Lamu.

Bw Athman anasisitiza kuwa malipo ya uanaharakati sio fedha bali ni kuona mageuzi yakitekelezwa au kufanyika katika yale yanayopiganiwa kupitia juhudi au kelele za wanaharakati.

“Kwanza kizazi cha leo hakitaki kujitolea kupigania jamii zao. Wengi ni waoga na wametawaliwa na anasa. Wamejitosa kwenye ulaji wa muguka, miraa na dawa za kulevya. Hawana muda na uanaharakati. Yaani hawataki kujitolea mhanga kusukumwasukumwa kwa ajili ya kuitetea jamii yao kama tulivyoshuhudia nyakati za wanaharakati wa zamani eneo hili kama vile marehemu Abubakar Khatib na wengineo,” asema Bw Ali.

Sababu nyingine inayopoesha uanaharakati Lamu ni jinsi ambavyo wanaharakati wamelemewa na majukumu ya kifamilia.

Bw Salim Omar, ambaye ni mwanaharakati wa zamani kisiwani Lamu, anaeleza kuwa uhitaji wa kifamilia ndio uliomfanya yeye binafsi kujitenga na uanaharakati kwani hata nafasi ya kutekeleza majukumu yampasayo mwanaharakati alikosa.

“Kwa sasa nimesalia kuupenda uanaharakati kwa moyo tu. Wasaa wa kushiriki kampeni za wanaharakati ndio sina kabisa. Niko mbioni kuitafutia na kuikimu familia yangu—mke na wanangu sita,” asema Bw Omar.

Wanaharakati wengine waliohojiwa na Taifa Leo, waligusia vitisho vya maisha yao ambavyo walidai hata baadhi ya viongozi wanaweza kutumia visivyo vyombo vya dola.

Hilo wanasema huwafanya kusalia nyuma katika kusukuma ajenda za uanaharakati eneo hilo.

Bw Ahmed Alwy, mwanaharakati wa zamani, anataja ukosefu wa ufadhili kuwa miongoni mwa vizingiti vinavyolemaza uanaharakati.

Bw Alwy anasema kampeni za wanaharakati mara nyingi huhitaji fedha.

“Kwa mfano ukitaka kutetea haki ya mja aliyedhulimiwa kupitia njia ya mahakama, ni wazi utahitaji fedha za kudhamini kesi kupitia wakili wa kusimama mbele ya mahakama. Hata kuwafikia wale unaowatetea pia wahitaji fedha au nauli ya kusafiria. Kama ufadhili hakuna, uanaharakati moja kwa moja unasalia kuwa ndoto tu,” asema Bw Alwy.

Pia anataja kwamba baadhi ya wanaharakati wa sasa wamekuwa vibaraka wa serikali, hivyo kusababisha mgawanyiko na ukosefu wa umoja na uwajibikaji miongoni mwa wanaharakati husika.

“Utapata hata yale mashirika machache yenye azma ya kufadhili uanaharakati pia yamekandamizwa serikalini kwani lazima yapitie kwa serikali, hasa za kaunti kwanza kabla ya kuwafikia wanaharakati au makundi ya kijamii. Yaani hakuna uhuru wala siri tena. Hili linapunguzia wanaharakati mori hasa endapo watahitajika kufokea serikali au utawala ulioruhusu ufadhili kuwafikia wanaharakati husika,” afichua.

Sababu nyingine kuu iliyojitokeza na inayolemaza uanaharakati Lamu ni kwamba baadhi ya wanaharakati walionelea heri kujitenga na uanaharakati hasa baada ya kufaulu kutajirika na kutosheka katika kipindi walipokuwa wakitekeleza shughuli hizo.