Wanaharakati wataka usalama uimarishwe Malindi

Wanaharakati wataka usalama uimarishwe Malindi

NA ALEX KALAMA

MASHIRIKA ya kutetea haki za kibinadamu kaunti ya Kilifi yamesisitiza haja ya kuimarishwa kwa usalama mjini Malindi ili kuboresha sekta ya utalii eneo hilo.

Kulingana na afisa wa shirika la Haki Yetu kaunti hiyo Bi Warida Zige, huenda visa vya utovu wa usalama vinavyoripotiwa kila mara vinachangia idadi ndogo ya watalii wanaozuru eneo hilo.

“Kwa sababu mji wa Malindi ni kitovu cha utalii na tukiona kuwa kuna hizi changamoto za utovu wa usalama, itaweza kutuathiri katika maswala ya wageni kutembelea maeneo yetu. Tumepata serikali mpya ya kaunti na tumeona serikali iliyopita baada ya miaka kumi ya ugatuzi hawajaweza kuweka mkazo kuhusu jambo hili. Kwa hivyo ni jambo la kuweza kuangaliwa kwa haraka iwezekanavyo,” alisema Bi Zige.

Anayehojiwa ni afisa wa shirika la Haki Yetu Kilifi Bi Warida Zige ambapo anazungumza kuhusu usalama kudorora Malindi. PICHA | ALEX KALAMA

Aidha mwanaharakati huyo alitaja maeneo ya Kisumu Ndogo na Maweni mjini humo kuwa baadhi ya sehemu zilizoathirika zaidi na utovu wa usalama.

“Tunaona hali ya usalama imeanza kuzorota hapa Malindi hususani maeneo ya Kisumu ndogo, Shella na Maweni. Na ni jambo la kusikitisha sana unakuta watoto wadogo ambao hawajafikisha miaka kumi na nane ndio wamekuwa wahuni wakukata watu mapanga. Na hii imeharibu sifa ya mji wetu imefanya hata wageni wanaogopa kuja kutembea Malindi, kwa sababu wanahofia usalama wao. Tutaka vitengo vya usalama viweze kuchukua hatua za kudhibiti jambo hili,” alisema Bi Zige.

Hata hivyo kwa upande wake Afia Swaleh afisa kutoka shirika la Muhuri amewataka wadau mbalimbali na taasisi za kiusalama kushirikiana kwa karibu ili kutatua changamoto hiyo.

“Tungependa kuona kuwa kutakuwa na kusemezana ama kutakuwa na mikutano yenye,washikadau tofauti tofauti tutaweza kukaa tuone tunafanya nini kupata suluhu. Kwa sababu jambo hili si la kuachiwa polisi pekee bali linahitaji ushirikiano ili kuhakikisha kuwa usalama unaimarika Malindi,” alisema Bi Swaleh.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi watakiwa kuunga mkono serikali ya Ruto

Nassir afunga majaa matatu ya taka

T L