Habari Mseto

Wanaharakati waweka wazi kile serikali inafaa kufanya kabla wanafunzi waruhusiwe shuleni

May 27th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

HUKU zikiwa zimesalia siku chache kabla ya hatima ya shule kufunguliwa kujulikana, Mtandao wa Wanawake wa Mombasa Wenye Imani – Mombasa Women of Faith Network – umetoa dukuduku lake kuhusu swala hilo.

Kulingana nao, sasa si wakati mwafaka wa wanafunzi kurudi shuleni kufuatia idadi kubwa ya visa vya ugonjwa wa Covid-19 vinavyoendelea kuthibitishwa kila siku tangu kisa cha kwanza nchini Machi 13, 2020.

Akizungumza na Taifa Leo mratibu wa mipango ya mtandao huo Bi Shamsa Abubakar amesema Jumatano ni hatari kuwarudisha wanafunzi shuleni wakati huu ambapo wakazi hawajazingatia kikamilifu kanuni na masharti ya kuzingatia ili kuepuka maambukizi.

“Bado tunaona watoto wanazurura mitaani bila maski; vipi walimu wataweza kuwahimiza kufuata masharti? ”akauliza mwanaharakati huyo.

Bi Abubakar amesema kabla ya kufungua shule, serikali inapaswa kuweka mikakati ya kuwapa hamasisho walimu kuhusiana na ugonjwa huo na kuwa tayari kupeleka vifaa vya kujilinda (PPE) katika shule kama maski na sanitaiza.

Aidha ameitaka serikali kuu kupitia Wizara ya Afya kuweka wazi takwimu za wagonjwa wa Covid-19.

“Tumechoka na siri za serikali, Covid-19 si ugonjwa wa zinaa hivyo haina haja kuwaficha wagonjwa,” amedai.

Kulingana naye, kuwekwa wazi majina ya wagonjwa wa Covid-19 kutasaidia wakazi wengine kuamini uwepo wa ugonjwa huo hatari.

Wakati huo huo amesema kuna haja ya serikali kutenga sehemu maalum ambazo wanafunzi wanaweza wakawekwa karantini kabla ya kuwaruhusu wajumuika katika shule zao.

“Serikali inapaswa kuwa imetenga fedha za kuwapeleka karantini wanafunzi hadi hali za afya zao zijulikane kabla ya kuruhusiwa kujumuika,” akasema.

Pia amesema wanafunzi wanaotoka katika kaunti zilizowekewa marufuku au zuio la watu ama kuingia au kuondoka, wawekewe mikakati itakayohakikisha wanasafiri bila tashwishi.

Kulingana na Wizara ya Elimu, serikali inapanga kufungua shule Juni 2020.