Habari Mseto

Wanaharakati wazimwa kufanya kikao kuhusu SGR

November 2nd, 2019 2 min read

Na ANTHONY KITIMO

MKUTANO uliotarajiwa kuhutubiwa na wanaharakati Yash Pal Ghai, David Ndii na Maina Kiai mjini Mombasa ulitibuka Jumamosi baada ya viongozi hao kuzuiwa kwa madai walitaka kuzua taharuki.

Wanaharakati hao walizuiwa kuingia katika Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa (TUM) ambapo walitarajiwa kuhutubia wakazi kuhusu masuala yanayowahusu likiwemo la uzorotaji wa uchumi kufuatia amri ya serikali ya kubeba mizigo yote kutumia reli ya kisasa (SGR).

Mwenyekiti wa shirika la kutetea haki za kibinadamu (Muhuri) Khelef Khalifa alisema wakuu wa chuo hicho waliwanyima ukumbi wakihofia vurugu zingezuka kutokana na mada zilizonuiwa kujadiliwa.

“Tunasikitika licha ya kulipia ukumbi huo, tumenyimwa ruhusa kuutumia na kunajua walipewa amri hiyo na baadhi ya wakuu serikalini. Hata hivyo, tutaendelea na mipango ya kupanga mkutano mwingine kama huu siku chache zijazo,” alisema Bw Khalifa.

Profesa Ghai alisikitika jinsi serikali ilinavyotekeleza katiba hii ambayo alichangia pakubwa kuiandika.

“Wakati wa kufanyia marekebisho ya katiba tunayotumia kwa sasa, tulikuwa na matumaini makubwa kuwa serikali itaitekeleza vilivyo ili ugatuzi uweze kufaidi wakazi wa kila kaunti. Lakini jinsi tunaona kaunti mbalimbali zikihujumiwa ni jambo la kusikitisha sana,” alisema Prof Ghai.

Wailaumu serikali

Wakiongea nje ya chuo hicho, wanaharakati hao walilaumu serikali kwa kuwanyanyasa ili wakome kuikosoa.

Dkt Ndii alisema amri ya serikali ya kubeba mizigo kutumia SGR ni kinyume na sheria kwani waagizaji mizigo wako na uhuru wa kuchagua njia inayowafaa.

“Tumekuwa tukisema kuwa mradi huo wa reli hauwezi kujilipia deni na mipango ya Halmashauri ya Bandari (KPA) na shirika la reli nchini kushinikiza wafanyabiashara kutumia ni kinyume cha sheria na tutaendelea kupinga hilo,” alisema Dkt Ndii.

Dkt Ndii alisema amri hiyo imesababisha kuzorota kwa uchumi wa watu wa Mombasa na sehemu nyingi ambazo zilikuwa zikitegemea matrela kujikimu.

Bw Kiai naye alisema wataendelea kubuni makundi katika kila kaunti ili kutetea dhidi ya unyanyasaji wa serikali.

“Siku ya leo tuko na ‘Okoa Mombasa’ ili kutetea wakazi dhidi ya dhuluma zinazoendezwa na serikali. Tutaenda katika kila kaunti kuhakikisha rasilmali zimelindwa dhidi ya tamaa ya mabwenyenye wachahce,” alisema Bw Kiai.