Habari Mseto

Wanaiba Kenya kisha kutorokea TZ, mahakama yaambiwa

April 11th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

HAKIMU mkuu Bw Francis Andayi ameamuru wanawake watatu na wanaume wawili wanaoshukiwa kuwa majambazi sugu na ambao walitorokea Tanzania kujificha nchini wazuiliwe kwa muda wa siku 15 kuhojiwa.

Na wakati huo huo, Jaji  Andayi aliamuru polisi wawasilishe mashtaka dhidi ya washukiwa hao katika muda wa saa 24 la sivyo atawaachillia kwa dhamana ili polisi wawachunguze wakiwa huru.

Bi Lavenda Akinyi Ogilo, Bi Teresa Richard, Bi Rose Richard, Bw Wycliffe Nyakundi Orwaru na Shimton Ambasa Khan waliamriwa wazuliwe katika kituo cha polisi cha Kilimani kuwasaidia maafisa wa polisi kuchunguza visa mbalimbali vya wizi wa mabavu.

“Punde tu washukiwa hawa wanapotekeleza uhalifu wao hutorokea nchi jirani ya Tanzania,” alisema Konstebo James Wanjohi wa idara ya upelelezi.

Hakimun alifahamishwa kwamba washukiwa hao wametambuliwa katika picha za CCTV ambapo wanaonekana wakiwa wamejihami na bastola.

“Punde tu wanapotekeleza uhalifu washukiwa hawa hutorokea nchi jirani ya Tanzania,” alisema Bw Wanjohi aliyeongeza , “kwa muda wa miaka mitatu tumekuwa tukichunguza mienendo ya washukiwa hawa watano.:

Korti ilikubalia ombi la polisi la kuzuiliwa kwa washukiwa hao kuhojiwa hadi Ijumaa.

Bidhaa mbalimbali zinazodaiwa zimeibwa na washukiwa hao zilipatikana. Polisi wametoa tangazo kwa umma kufika kuandikisha taarifa kuhusu bidhaa walizopoteza.