Habari za Kitaifa

Wanajeshi sasa kupelekwa kaunti zote 47, na hizi ndizo sababu

Na BENSON MATHEKA June 30th, 2024 1 min read

MAAFISA wa Jeshi la Kenya (KDF) watapelekwa katika kaunti zote nchini kuzima uasi unaoweza kuchipuka kufuatia maandamano ya Jumanne na Alhamisi, Waziri wa Ulinzi Aden Duale ametangaza.

Bw Duale anasema  kutumwa kwa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) katika kaunti zote 47 kutasaidia polisi kurejesha utulivu baada ya maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha ambao Rais Ruto amerudisha bungeni ufutwe.

Katika ilani mpya ya gazeti la serikali iliyochapishwa kufuatia maagizo ambayo yalitolewa na Jaji Lawrence Mugambi,Alhamisi, Waziri Duale anasema kuwa maafisa wa KDF watalinda miundomisingi ya serikali katika kaunti zote huku wakisaidia polisi kuzima machafuko.

Waziri Duale alisema kuwa operesheni hiyo itaisha mara tu hali ya kawaida itakaporejea nchini kote.

 “Kutoka na vtisho kwa usalama wa taifa vilivyopangwa na kuratibiwa kupitia majukwaa mbalimbali ya mtandao, watapelekwa( KDF) kaunti arobaini na saba ndani ya Jamhuri ya Kenya ambako kuna miundombinu muhimu ili kusaidia Huduma ya Kitaifa ya Polisi kuokoa maisha , kulinda usalama wa ndani wa Serikali, kulinda mali na pia kudumisha sheria na utulivu.

“Masharti ya majukumu yao  yatakuwa kwa  viwango vya kikatiba, Vifungu 238 (1) na (2) vya Katiba ya Kenya, 2010, mahitaji ya kisheria na kanuni zinazotolewa katika vifungu vya 3, 8 (2) , 34 (1), 34 (3) na 35 ya Sheria ya Majeshi ya Ulinzi ya Kenya,” ilisema  sehemu ya ilani ya Duale

Tangazo la awali la kutumwa kwa KDF lilifanywa Jumanne, Juni 25 na kuidhinishwa na Bunge Jumatano, Juni 26.

Hatua hiyo ilipingwa na Chama cha Wanasheria nchini (LSK) ambacho kilidai ilikuwa kinyume cha katiba.

Hata hivyo, mahakama iliamua kwamba  kupelekwa kwa wanajeshi ni muhimu kufuatia uvamizi katika  Majengo ya Bunge na ikaagiza waziri  kuchapisha mwongozo wa kupelekwa kwao, majukumu yao na maeneo wanayopaswa kuhudumu ndani ya siku mbili.