Wanajeshi wa Ulinzi Warriors watupia jicho Ferroviario baada ya kuumwa na Cobra vikapuni

Wanajeshi wa Ulinzi Warriors watupia jicho Ferroviario baada ya kuumwa na Cobra vikapuni

Na GEOFFREY ANENE

ULINZI Warriors watakuwa na mechi ya kufa-kupona dhidi ya Ferroviario Beira kwenye mashindano ya mpira wa vikapu ya zoni ya Mashariki maarufu kama Road to BAL Elite 16 nchini Afrika Kusini leo alasiri.

Wanajeshi hao kutoka Kenya walianza kampeni ya kufuzu kushiriki michuano ya Afrika vibaya walipopoteza 77-67 dhidi ya Cobra Sports kutoka Sudan Kusini katika mechi hiyo ya Kundi H2 ukumbini Wembley, Johannesburg mnamo Desemba 8.

Mabingwa hao wa Kenya walizoa robo ya kwanza 17-13 kabla ya kupoteza tatu zilizofuata 23-15, 21-20 na 20-15 na mechi hiyo. Timu mbili za kwanza kutoka kundi hili pamoja na idadi sawa kutoka Kundi H1, ambalo liko na Cape Town Tigers (Afrika Kusini), New Star (Burundi) na Matero Magic (Zambia), zitaingia nusu-fainali huku wavuta-mkia katika makundi yao wakiaga mashindano.

“Mchezo wetu dhidi ya Cobra ulikuwa mzuri licha ya kupoteza mchuano huo. Tumekuwa na kikao na kuangalia wapi tulifanya vibaya na tunasubiri kwa ari kumenyana na Ferroviario,” meneja wa timu ya Ulinzi Warriors, Stephen Bartilol ameeleza Taifa Leo mnamo Alhamisi.

Ameongeza, “Hatujawahi kukutana na timu hiyo kutoka Msumbiji, lakini tulipata kuwaona walipocheza dhidi ya Cobra mnamo Jumatano. Itakuwa mechi ngumu. Uchunguzi wetu kuwahusu umefichua kuwa asilimia 80 ya wachezaji wao wako katika timu ya taifa. Hata hivyo, hilo halitutii wasiwasi.” Washindi wa medali ya dhahabu, fedha na shaba watajikatia tiketi kushiriki mashindano ya Afrika jijini Kigali, Rwanda mwaka 2022.

You can share this post!

Wakazi walalamika unyakuzi bandarini

Junet amkataa Wanjigi

T L