Habari Mseto

Wanakijiji waua mshukiwa wa unajisi

April 11th, 2018 1 min read

Na NDUNGU GACHANE

WANAKIJIJI katika Kaunti ya Murang’a walimuua mwanafunzi wa kidato cha kwanza aliyedaiwa kumnajisi msichana wa miaka 12 kabla kumnyonga kwa tai ya shule hadi akafariki.

Wakazi hao waliojaa hasira kutoka kijiji cha Gituto, eneo bunge la Kiharu, walimpiga mawe Duncan Wakahiu kabla ya kumchoma baada ya msichana huyo kupatikana ndani ya chumba chake.

Msichana huyo alikuwa amesakwa na jamaa zake kwa saa kadha kabla kupatikana ndani ya chumba hicho.

Kulingana na nyanyake Lucy Wambui, binti huyo alikuwa ametumwa dukani na dadake alipokutana na kijana huyo aliyemvuta hadi chumbani akamnajisi na kisha kutumia tai yake ya shule kumnyonga.

Bi Wambui alisema kuwa baada ya mjukuu wake huyo mwingine kurejea nyumbani na kumkosa dadake walianza kumtafuta. Ni hapo marafiki walimfahamisha kwamba alikuwa chumbani kwa kijana huyo.

“Watoto wengine walituambia kuwa Wakahiu alikuwa amemuomba amsaidie kubeba mizigo fulani chumbani mwake. Kijana huyo kisha akawataka watoto hao kuondoka akisema kwamba atampeleka nyumbani,” nyanya huyo alieleza.

Kijana huyo alikuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya Gituto huku marehemu akiwa darasa la tano katika shule ya Gitige.

Bi Wambui alisema kuwa baada ya kufahamishwa alikokuwa mjukuu wake walifululiza hadi kwa kijana huyo na kupata nyumba imefungwa. Babake mshukiwa alilazimika kufungua lango la chumba cha kijana huyo na hapo wakampata msichana akiwa amenyongwa.

Wanakijiji walianza msako na walipompata mshukiwa walimuua.

Akithibitisha kisa hicho, mkuu wa polisi Kahuro Bw David Kandie alisema mshukiwa alikuwa amechomwa kiasi cha kutotambulika.

Aliwaomba wakazi kusita kuchukua sheria mikononi mwao dhidi ya washukiwa.

“Tumeanzisha uchunguzi kubaini matukio yalivyojiri na iwapo yeyote atapatikana na hatia atakabiliwa vilivyo kisheria,” akasema Bw Kandie.