Michezo

Wanamagongo wa Butali wafalme Parklands Open

February 26th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

WAFALME wa magongo nchini Butali Warriors walijitahidi kiume na kutawazwa mabingwa wa shindano la Parklands Open lililoandaliwa wikendi iliyopita katika uwanja wa Parklands jijini Nairobi.

Butali ya kocha Dennis Owoka ilibeba taji hilo baada ya kushinda Wazalendo mabao 2-1 katika fainali ya kusisimua.

Klabu ya Butali inayojivunia kusajili wachezaji kadhaa kujiandalia msimu mpya wa Ligi Kuu, ilivuna ufanisi huo kupitia mabao ya sajili mpya Calvin Kanu na Moses Ademba.

Naye Dennis Mwanzo alitingia Wazalendo bao la kufuta machozi.

“Sina shaka kusema kwamba michezo ya kipute hicho ilisaidia washiriki kujipima nguvu kabla ya mechi za ligi za msimu mpya kukunjua jamvi,” alisema nahodha wa Parklands, Kelly Adolwa.

Kuikomoa Nairobi Simba

Butali ilifuzu kushiriki fainali ilipokomoa Nairobi Simba 3-1 kwenye nusu-fainali ya kwanza nayo Wazalendo ilijinyakulia tiketi ya kusonga mbele baada ya kulemea Sailors 1-0.

Kwenye robo-fainali, Parklands Sports ilisakamwa 2-0 na Nairobi Simba, Wazalendo iliipiga Sailors 1-0, miamba Kenya Police wakapepetwa 1-0 na Greensharks nao wafalme wa Kenya, Butali wakakung’uta Parkroad 2-0.