Habari Mseto

Wanamazingira wa Kenya wajiunga na wenzao duniani kuhimiza umuhimu wa uhifadhi mazingira

October 3rd, 2019 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

WAHIFADHI mazingira wa Kenya wamejiunga na wenzao kutoka nchi mbalimbali katika mjadala unaoendelea kuhusu ongezeko la viwango vya joto duniani.

Wahifadhi mazingira hao sasa wameitaka serikali kupiga marufuku matumizi ya mafuta (fuel) yanayotoa hewa aina ya kaboni.

Kulingana na ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa (UN) iliyotolewa juma moja lililopita, kuna ongezeko kubwa la joto ambalo linasababisha kuyeyuka kwa barafu katika maeneo yaliyohifadhiwa na ongezeko la asidi.

Madhara hayo yanasababishwa na ongezeko la aina hiyo ya hewa.

Wanamazingira hao wamesema kuwa Kenya si ya kipekee katika swala hili na kwamba madhara ya uchafuzi huo wa mazingira yataiathiri kama nchi zingine.

“Inasikitisha kwamba mataifa yenye utajiri mkubwa yanaendelea kuachilia gesi ambazo zina madhara kwa ulimwengu mzima ilhali yana uwezo wa kutafuta njia mbadala za nishati,” alisema mratibu wa Integrated Lake Basin Management (ILBM) Bw Jackson Raini.

Mwanamazingira mwingine Bw James Wakibia alisema kuwa uchafuzi wa hewa unaweza kulaumiwa kwa kiangazi ambacho kimekuwa kikishuhudiwa katika sehemu mbalimbali nchini pamoja na upungufu wa chakula.

“Kuna njia nyngi ambazo tunaweza kuzikumbatia ili kupunguza uchafuzi huo. viwanda ambavyo vinatoa gesi ya kaboni pia vinafaa kufungwa,” alisema Bw Wakibia.