Wanamuziki wajiandaa kuvuna vinono siasa za 2022 zikinoga

Wanamuziki wajiandaa kuvuna vinono siasa za 2022 zikinoga

Na NICHOLAS KOMU

WANAMUZIKI Mlima Kenya wameanza kuchukua mirengo tofauti ya kisiasa, uchaguzi mkuu wa 2022 unapokaribia na kampeni za ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) zinapozidi kushika kasi.Kwa wanamuziki hao, ambao wanaimba nyimbo za densi na zile za injili, huu ni wakati mwafaka wa kuonyesha mirengo wanayoegemea.

Baadhi wamesema miegemeo hiyo inatokana na mitazamo yao kisiasa, huku wengine wakieleza nia yao ni kujifaidi kifedha.Hata hivyo, wengi walisema lengo lao ni kupata pesa.

“Inategemea ikiwa mwanamuziki husika anaongozwa na imani zake kisiasa ama analenga kujifaidi kifedha. Lengo kuu ni kuwa mwishoni, ni kazi kama zile zingine,” akaeleza mwanamuziki Muigai wa Njoroge.

Wanamuziki hao wana ufuasi mkubwa katika ukanda huo kutokana na uwezo wa kipekee kwenye utunzi wa nyimbo. Ni hali inayotarajiwa kuwashawishi wapigakura kuhusu mrengo watakaounga mkono.

Kutokana na umaarufu huo, wanasiasa wengi wako tayari kutumia fedha kuwashawishi wanamuziki kuwafikia wapigakura na wafuasi wao kwa njia ya nyimbo.

Mwanamuziki Ben Githae anatajwa kuwa mfano bora kuhusu jinsi muziki wa lugha asili ya Gikuyu ulivyo na uhusiano mkubwa na siasa katika eneo la Kati.

Wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Agosti 2017, Bw Githae alitunga wimbo ‘Tano Tena’ ulioisifia serikali ya Jubilee.Kutokana na umaarufu mkubwa wa wimbo huo, Bw Githae alikuwa akialikwa katika karibu kila mkutano wa kampeni za Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto.

Baadaye, alitunga wimbo ‘Wembe ni Ule Ule’ kuimarisha kampeni za Jubilee kutokana na marudio ya uchaguzi wa urais Oktoba 2017.Kwa sasa, wanasiasa wanawatafuta wanamuziki kutunga nyimbo za kuwapigia debe miongoni mwa wenyeji katika ukanda huo wenye idadi kubwa ya wapigakura.

Wale wanatakaofaulu watajumuishwa kwenye mikutano ya kisiasa ya viongozi hao kati ya shughuli zingine za kuwapa umaarufu. Majuzi, Dkt Ruto alikutana na wanamuziki kadhaa kutoka jamii ya Gikuyu, kwenye hatua inayoonekana kama mkakati wa kuwatumia watumbuizaji hao kuendeleza ushawishi wake wa kisiasa katika ukanda wa Mlima Kenya.

Wanamuziki hao waliongozwa na Bw Njoroge.Bw Njoroge aliiambia ‘Taifa Leo’ kwamba lengo kuu la mkutano huo lilikuwa “kuangazia maslahi ya wanamuziki.”

Alisema hili ni kwa kuwa Dkt Ruto amekuwa akijali masuala yanayowaathiri.Licha ya kiini halisi cha mkutano huo kutojitokeza wazi, hatua ya kumtumia Bw Njoroge inaonekana kama mkakati wa Dkt Ruto kuimarisha azma yake ya kuwania urais.

Katika siku za hivi karibuni, mwanamuziki huyo amekuwa akitunga nyimbo za kuukashifu utawala wa Jubilee na Rais Kenyatta.Hili ni kupitia nyimbo kama “Mbari ya Kimeendero” (Ukoo wa Wakandamizaji), “Tukunia” (Wasaliti) kati ya nyingine.

You can share this post!

Wapinzani taabani Ruto akiidhinishwa kuongoza Wakalenjin

BENSON MATHEKA: Museveni amegeuza Uganda kuwa mali ya...