Habari Mseto

Wananchi kusubiri zaidi bei ya unga kushuka

May 23rd, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Wakenya watazidi kungoja kupata unga wa bei ya chini kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Wizara ya Kilimo na Hifadhi Kuu ya Chakula (SFR).

Wizara hiyo na bodi ya SFR zimetofautiana kuhusiana na shirika linalofaa kutoa mahindi hayo. Bodi ya SFR iliudhishwa na tangazo la wizara hiyo katika magazeti kuhusiana utaratibu wa kutoa magunia milioni tatu kutoka kwa Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB), na kushutumu wizara hiyo kwa kuingilia wajibu wake.

“Tangazo lilichapishwa magazetini halistahili kwa sababu lilichapishwa na watu wasio, ambao hawasimamii mahindi SFR,” alisema Noah Wekesa, mwenyekiti wa SFR.

Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri alikutana na watengenezaji wa unga mwezi jana na kukubali kutoa mahindi ya bei ya chini kwa lengo la kudhibiti ongezeko la bei ya unga.

Unga wa mahindi unauzwa kwa Sh120 kwa kilo mbili, kutoka Sh86.50 Machi kutokana na upungufu wa mahindi sokoni.

Viwanda hivyo vinanunua gunia la mahindi kwa Sh3, 400 kutoka Sh2, 700 Februari. Lakini serikali inatarajiwa kuuza magunia milioni tatu kwa Sh2, 300 kwa kila moja, hatua inayotarajiwa kupunguza bei ya unga kwa wananchi.

Kulingana na Dkt Wekesa, mahindi yote yaliyo NCPB yanasimamiwa na SFR, hivyo shirika hilo linafaa kuzungumzia utaratibu wa kutoa mahindi hayo.