Makala

Wananchi wa Haiti wakosa subira, wataka polisi wa Kenya kumaliza wahalifu chapchap


WIKI sita baada ya kundi la polisi wa Kenya kutua nchini Haiti kusaidia polisi wa nchi hiyo kudhibiti magenge ya wahalifu, uwezo wao kutekeleza kibarua hicho umeanza kutiliwa shaka.

Viongozi, raia na wanahabari nchini humo sasa wamegeuka na kuwasuta Wakenya hao  wakiwataja kama “waigizaji” na “watalii” wasiosaidia chochote huku magenge yakiendelea kuwahangaisha raia.

Raia wengi wa Haiti walijawa na matumaini makubwa kundi la kwanza la polisi 200 kutoka Kenya lilipotua jijini Port-au-Prince mnamo Juni 25.

Maafisa hao walionyesha  mbwembwe nyingi wakivalia helmeti, magwanda ya kijeshi, wakibeba silaha zao na kuinua bendera ya Kenya.

Hali ilikuwa sawa na hiyo kundi la pili la Polisi hao lilipowasili nchini humo majuma matatu yaliyofuata.

Kulikuwa na matumaini kwamba polisi wa Kenya wangeleta nguvu mpya kwa Polisi wa Kitaifa wa Haiti (PNH) kupambana na magenge ya wahalifu ambao wamehangaisha jiji kuu Port-au-Prince na maeneo mengine nchini humo kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.

Kituo cha Redio cha Independante FM kiliweka ujumbe wa kuwakaribisha Wakenya hao nchini humo uliosema hivi:

“Haiti ni nchi ya Waafrika wote. Kwa kuwa ninyi ni weusi, Haiti ni nyumbani kwenu…… Enyi wanajeshi wa Kenya mko nyumbani na tunawakaribisha kusaidia kupambana na magenge haya ambayo yametuzuia kuishi katika nchi yetu.”

Lakini sasa, raia wengi wa Haiti wanahisi kupoteza imani kwamba polisi hao wa Kenya na wenzao wa Haiti hawajachukua hatua za haraka kuzima magenge ya wahalifu, wakuu wao  na kuvamia maficho yao.

Huku wakitumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, raia wanasema wanataka “vitendo sio maneno matupu” na “matokeo halisi”.

Wakosoaji wanasema licha ya doria za pamoja zinazoendeshwa na polisi wa Kenya na wenzao wa Haiti jijini Port-au-Prince ambako wamekabiliana kwa risasi na magenge, wahalifu hao bado wanadhibiti maeneo ya kusini na kaskazini mwa jijini na viungani mwake.

Tangu polisi wa Kenya watue Haiti wanachama wa magenge ya wahalifu wamevamia vituo vya polisi na kuendelea kuwahangaisha watu katika barabara kuu jijini humo na miji mingine.

Kuna hisia nchini Haiti kwamba polisi wa Kenya wamejivuta kuhakikisha kuwa uwepo wao unaonekana.

“Wakenya hawa wanasubiri nini kabla ya kuchukua hatua dhidi ya majangili hao,” kituo cha habari cha AyiboPost kikauliza kwenye taarifa kilichoweka katika mtandao wa X mnamo Julai 11, majuma mawili baada ya kundi la kwanza la maafisa wa kutua Haiti.

Wiki mbili baada ya mtandao wa habari kwa jina “Le Filet Info” nao ukasema hivi: “Uwepo wa polisi wa Kenya nchini Haiti haujasaidia kushtua wahalifu hao. Wanaendelea kuwaua raia.”

Kikosi cha Kenya tayari kimepata majeruhi ya kwanza tangu kilipowasili Haiti.

Mnamo Julai 30, mmoja polisi hao alipata jeraha la risasi begani maafisa hao walipokabiliana na wahalifu wa genge moja la wahalifu jijini Port-au-Prince.

Siku hiyo Mkuu wa Polisi Haiti Rameau Normil, akiandamana na kamanda wa kikosi cha Kenya Godfrey Otunge, walionekana kujibu habari mbaya kuhusu maafisa wao kwa kutangaza kuwa “majangili” 100 waliuawa katika operesheni ya pamoja na vikosi hivyo viwili vya polisi.

Hata hivyo, kauli kama hizo hazijasaidia kurejesha imani ya umma kuhusu ufanisi wa juhudi za vikosi hivyo katika kulemaza wahalifu nchini Haiti.

Huku polisi wa Kenya wakiendelea kukosolewa kwa kushindwa kuwadhibiti wahalifu “haraka ilivyotarajiwa” kaimu Waziri Mkuu Garry Conille amewaambia wanahabari kwamba anaunga mkono usaidizi ambapo Wakenya hao wametoa kwa polisi wa Haiti.

Hata hivyo, akasema; “Tunahitaji usaidizi… japo unakuja polepole na rais wa Haiti wanaonekana kuchoka kusubiri.”

Lakini kiongozi huyo alifafanua kuwa wajibu wa polisi wa Kenya ni kutoa usaidizi huku wakiandamana na polisi wa Haiti –  “sio kuendesha operesheni za kiusalama kivyo.”

Hata hivyo, viongozi wa makundi ya wahalifu wameonekana kuwakaidia polisi wa Kenya.

Siku chache baada ya kundi la kwanza la maafisa 200 kuwasili Haiti, Jimmy “Barbecue” Cherizier, kiongozi wa kundi la “Viv Ansanm” alitoa kauli za kudharau polisi hao wa Kenya.

“Hizi ndizo risasi zitakazotumiwa kupambana na Wakenya. Tunataka kuwaambia kwamba hawatatuweza,” Barbecue na wanachama wa genge lake wakasema kwenye video iliyodumu kwa dakika nane. Walionekana wakisakata densi katika ngome yao ya Delmas 9 huku wakiinua juu bunduki zao hatari.

Viongozi wengine wa magenge ya wahalifu akiwemo Wilson “Lanmo Sanjou” Joseph, kiongozi wa genge la “400 Mawozo” na kiongozi mwingine kwa jina “Ti Bebe Bougoy” wamekuwa wakionekana katika video wakiwakemea maafisa wa Haiti na polisi wa Kenya.

Wao hufanya hivyo huku wanachama wao wakiendesha mashambulio dhidi ya raia.

Kikosi hicho cha polisi wa Kenya kilitumwa nchini Haiti chini ya idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kwa lengo la kurejesha usalama nchini humo.