Bambika

Wanandoa maarufu na mastaa Pascal Tokodi na Grace Ekirapa waachana

January 24th, 2024 2 min read

RAJAB ZAWADI NA FRIDAH OKACHI

MIEZI kadhaa baada ya ndoa ya Philip Karanja maarufu kama Director Phil, na mwigizaji Kate Actress kusambaratika, na kulazimika kujitokeza kutangaza talaka yao, ndoa nyingine ya mastaa mashuhuri imetibuka.

Mtandao wa Nairobi News umethibitisha ndoa ya mwigizaji na mwimbaji Pascal Tokodi na aliyekuwa mtangazaji wa kipindi cha NTV Crossover Grace Ekirapa, hawaishi pamoja.

Wanandoa hao waliokuwa wenye furaha, walifunga ndoa Oktoba 2020 katika sherehe ya kipekee.

Kulingana na taarifa ni kuwa wawili hao wamekuwa wakikabiliwa na matatizo ya muda mrefu hadi pale ndoa ilipovunjika Novemba 2023.

Rafiki wa karibu, ambaye alipata fursa ya kuhudhuria harusi yao ambayo ilikuwa ya kisiri alifichua kwamba kudumisha maisha ya kifahari ilichangia utengano wa wawili hao.

Tokodi ndiye aliyekuwa akitegemewa, huku Ekirapa akisalia kuwa mke nyumbani akitunza binti yao mchanga.

Wanandoa hao wanakabiliwa na changamoto licha ya kuweka machapisho yao kwenye mitandao ya kijamii kuthibitishia wafuasi wao kuwa ndoa yao haikuwa na dosari.

“Kwa muda wa miezi miwili sasa, Pascal na Grace hawajakuwa wakiishi pamoja. Waliachana Novemba 2023. Pascal alirejea kwenye maskani yake huko Karen alipokuwa akiishi kabla ya kukutana naye Grace. Grace amesalia Limuru walipokuwa wakiishi pamoja,” aliambia  Nairobi News.

Kulingana na rafiki huyo, chanzo cha ndoa yao kuvunjika ni kutokana na changamoto za kifedha.

 “Tangu alipoolewa, Grace amekuwa na tatizo kuhusu marafiki wa Pascal. Nilikuwa mmoja wa marafiki ambao nilikatiza uhusiano na wao; tulianza kuongea hivi majuzi. Hakutaka Tokodi afanye ushirikiano na King Kaka, alihisi mumewe anatumiwa,” alidai rafiki huyo.

Hakuna mmoja wao aliyemiliki gari tangu wafunge ndoa. Na walionelea kuwekeza.

“Mimi na Pascal ni marafiki wa karibu, na alichoniambia ni kwamba alipendelea kununua gari lenye bei nafuu, ambalo ni Demio ili kuanza maisha. Lakini Grace alishauri wanunue gari kubwa zaidi. Hivyo ndivyo Pascal alichukua mkopo na kununua Mazda CX-5 kwa Sh1.9 milioni na ungemwona akizunguka nalo. Na analipia mkopo huo,” alisema rafiki huyo.

Wanandoa hao waliishi kwanza Kitengela na, wakati fulani, waliwekeza maelfu ya pesa kukarabati nyumba ya kukodisha ili kukidhi viwango vyao vya maisha. Baada ya muda, waliamua kubadili makazi na kuhamia Limuru, ambapo nyumba hiyo ilifanyiwa ukarabati tena.

“Grace alichoka kuishi Kitengelea na kupendekeza wahamie Limuru kwa sababu alitaka kuwa karibu na dada zake. Walikarabati tena nyumba, kumbuka Pascal ndiye anayesimamia bili zote kwa sababu Grace hana kazi. Msukumo wa kuishi maisha ya juu yenye bei ghali ilikuwa tatizo kudumishwa na Pascal.”

Wakati wa kupiga simu ili watoe maoni, Grace aliiambia Nairobi News jambo hilo hawezi kuzungumza na mtu wa nje.

“Simu hii imenipata kwa mshangao iwapo tuko pamoja au la. Sidhani kama ni jambo ambalo ningependa kuzungumza na mtu wa nje.”

Tokodi pia alijibu habari hizo akidai kuwa wako sawa.

“Kwa kweli tuko sawa. Lakini asante kwa kuuliza. Iwapo utampigia simu Grace atakupa jibu sawia na hili. Tuko sawa,” aliongeza Tokodi.