Habari Mseto

Wanane washtakiwa kwa kukaidi agizo la kusitisha ujenzi Westlands

July 1st, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WAFANYAKAZI wanane katika jengo ambalo ustawishaji wake ulikuwa umesimamishwa na mamlaka ya kitaifa ya ujenzi (NCA) walishtakiwa Jumanne.

Michael Nyagah (kulia pichani), Sirus Malenya, Broadrack Atitu, Megan Achieng, Victor Salano, Nathaniel Michael, Mary Waithera na Yohanes Kuflu walifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Bernard Ochoi katika mahakama ya Milimani, Nairobi.

Walikanusha shtaka la kukaidi agizo la NCA kusimamisha ujenzi wa jengo moja katika eneo la Westlands Nairobi.

Wanane hao walikana kwamba mnamo Juni 2020 walikaidi agizo la afisa kutoka NCA aliyekuwa anachunguza utaratibu wa ujenzi wa jumba lililoko karibu na ya Matunda.

Shtaka lilisema wanane hao walikaidi agizo wasitishe ujenzi wa jengo husika.

Mahakama ilifahamishwa washtakiwa waliendelea na ujenzi licha ya notisi kutoka NCA ikiwataka wasimamishe ujenzi.

Washtakiwa waliomba waachiliwe kwa dhamana huku wakimweleza hakimu “tulikuwa nje kwa dhamana ya Sh20,000 tuliyopewa na polisi; twaomba utuachilie kwa masharti sawa na hayo.”

Hakimu mwandamizi Bw Bernard Ochoi aliwaachilia washtakiwa kwa dhamana ya Sh100,000 pesa taslimu na kuamuru kiongozi wa mashtaka awape nakala za ushahidi.

Kesi itatajwa baada ya wiki mbili.