Wanaodai Magufuli aliuawa kwa sumu wajitokeze – Rais Suluhu

Wanaodai Magufuli aliuawa kwa sumu wajitokeze – Rais Suluhu

Na LEONARD ONYANGO

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amepuuzilia mbali madai ambayo yamekuwa yakienezwa katika mitandao ya kijamii kuwa mtangulizi wake Dkt John Pombe Magufuli aliuawa kwa sumu.

Rais Suluhu aliyekuwa akihutubia bunge la Tanzania jijini Dodoma Alhamisi, aliwataka wanaoeneza madai hayo kujitokeza kuandikisha taarifa kwa maafisa wa polisi wa Tanzania kuhusu wanachokijua.

“Madaktari wetu walitwambia kuwa mpendwa wetu Rais Magufuli alifariki kutokana na ulegevu wa moyo, tatizo ambalo amekuwa nalo kwa kipindi cha miaka 10.

“Lakini kumekuwa na kundi la watu mitandaoni ambao wamekuwa wakidai kuwa aliuawa kwa kuwekewa sumu kwa lengo la kuwagawanya Watanzania. Ikiwa wanaamini madai hayo ni ya kweli wajitokeze waanbdikishe taarifa,” akasema Rais Suluhu.

Magufuli alifariki ghafla Machi 17, mwaka huu, baada ya kuugua kwa chini ya mwezi mmoja.

“Ninawahimiza Watanzania kutumia mitandao kiungwana. Wanaoeneza madai ya uongo wanadhani kwamba wamejificha lakini tutawapata hivi karibuni,” akasema Rais Suluhu.

Katika hotuba yake, Rais Suluhu, vilevile, alivitaka vyombo vya habari kuendesha shughuli zao kwa uwajibikaji.

“Hakuna uhuru wa kidemokrasia usiolindwa na kusimamiwa na sheria, taratibu na kanuni,” Rais Suluhu akaambia bunge lililokuwa limejawa mbwembwe na shamrashamra.

Hiyo ilikuwa hotuba ya kwanza kwa Rais Suluhu kuhutubia bunge la Tanzania tangu alipoapishwa kuongoza taifa hilo la Afrika Mashariki kufuatia kifo cha Magufuli.

Katika kile huenda kikafurahisha upinzani, Rais Suluhu alisema kuwa analenga kukutana na viongozi wote wa upinzani “ili kwa pamoja tuweke mwelekeo wa kuendesha shughuli za kisiasa zenye tija na maslahi kwa taifa”

Mapema mwezi huu, kiongozi wa upinzani Freeman Mbowe aliomba kukutana na Rais Suluhu ili kujadili masuala muhimu ya kitaifa.

Rais Suluhu Alhamisi, aliorodesha baadhi ya mambo ambayo serikali yake inalenga kutekeleza ndani ya miaka mitano ijayo, ikiwemo kuboresha huduma za afya, miundomsingi, maji, nishati, elimu, haki mahakamani kati ya mengineyo.

You can share this post!

Wakili Yano asema atakuwa akiuliza kuhusu hisia za Rais

UDA yapinga talaka