Wanaodaiwa kusambaza ujumbe wa uchochezi wapata bondi

Wanaodaiwa kusambaza ujumbe wa uchochezi wapata bondi

NA TITUS OMINDE

WANAFUNZI tisa wa Chuo Kikuu cha Moi waliokamatwa kwa kuhusika katika usambazaji wa karatasi za uchochezi kupitia mtandao wa kijamii wa Whatsapp, wamekabiliwa na mashtaka matatu ya kueneza habari za uongo ili kuzua hofu kabla ya uchaguzi mkuu wiki ijayo.

Wanafunzi hao walipigwa dhamana ya Sh1 milioni kila mmoja na mdhamini wa kiwango sawa.

Katika shtaka la kwanza Ronald Odhiambo Ochieng, Martin Rodgers, Josphat Chacha, Ian Muibanda, Brian Kipkorir Keter, Dennis Salim Wakhanya, Beatrice Wangari Kumari, Samuel Otieno na Ann Aoko walishtakiwa kwa kuchapisha habari za uongo na matumizi mabaya ya kompyuta kinyume na Sheria ya Uhalifu wa Mitandao 2018.

Mahakama iliambiwa kuwa mnamo Julai 29 katika chuo hicho kilichoko Kaunti Ndogo ya Kesses, Kaunti ya Uasin Gishu, pamoja na wengine ambao hawakufika kortini, walichapisha habari ambazo zilikuwa za uongo kwa kutumia simu zao za rununu na kuchapisha habari za uongo zilizozua hofu na wasiwasi miongoni mwa Wakenya.

Habari zilizokuwa kwenye vijikaratasi zilionya jamii fulani kuondoka Uasin Gishu kabla ya uchaguzi wa wiki ijayo ikiwa hawatampigia kura mgombeaji fulani wa urais.

Katika shtaka la pili walishtakiwa kwa matumizi mabaya ya kompyuta na uhalifu wa mtandao sheria ya 2018 ambapo walionya jamii zinazoishi Rift Valley kuhakikisha wanampigia kura naibu wa rais William Ruto la sivyo watafurushwa kutoka eneo hilo.

Mwendesha mashtaka aliiambia mahakama kuwa matamshi ya mshtakiwa yalikusudiwa kusababisha hofu, fujo na vurugu miongoni mwa wananchi.

Shtaka lao lilisema kuwa washtakiwa walitumia taarifa za uongo kuzua hofu ili kushawishi mchakato wa upigaji kura siku ya Jumanne kinyume na sheria ya makosa ya uchaguzi ya mwaka 2016.

Wakiwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Eldoret Mogire Onkoba wote walikana mashtaka.Wanafunzi hao ambao hawakuwakilishwa na mawakili waliiomba mahakama kuwaachilia kwa masharti nafuu ya bondi.

“Ninatoka katika familia maskini, nategemea wazazi wangu ambao wanatatizika kunilipia karo na hawataweza kunilipia bondi kubwa,” mmoja wa washtakiwa aliambia mahakama.

Wakili wa serikali David Fedha hakupinga kuachiliwa kwao kwa dhamana.

Bw Fedha aliiambia mahakama kuwa kutokana na ukweli kwamba walikuwa wanafunzi ndiyo maana hakupinga kuachiliwa kwa dhamana, walakini aliitaka mahakama kuwaachilia kwa masharti magumu ya bondi kutokana na aina ya uhalifu.

“Serikali inaelewa hawa ni wanafunzi ndio maana sijapinga kuachiliwa kwao kwa dhamana. Hata hivyo, naomba masharti makali ya dhamana,” Bw Fedha aliambia mahakama.

Mahakama iliamuru kila mshtakiwa aachiliwe kwa bondi ya Sh1m na mdhamini sawa na huyo au dhamana mbadala ya pesa taslimu Sh500,000 kila mmoja.

Kesi hiyo itatajwa Agosti 22 kwa maelekezo zaidi.

  • Tags

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Usichague wenye ndimi telezi bali unaowaamini

Uchaguzi kuzima nyota za wanasiasa maarufu

T L