Wanaoendeleza ukeketaji Lamu wazimwa

Wanaoendeleza ukeketaji Lamu wazimwa

NA KALUME KAZUNGU

KAMPENI dhidi ya ukeketaji ambayo imekuwa ikiendelezwa na wanajamii na maafisa wa utawala kwenye vijiji mbalimbali vya Lamu imesaidia kupunguza tatizo hilo kwa asilimia 90.

Miaka kadha iliyopita, wasichana wengi hasa kutoka kwa jamii ndogo za Waboni na Orma wanaoishi Lamu walikuwa wakipashwa tohara na kisha kulazimishwa ndoa za mapema.

Visa vingi vya aina hiyo vilikuwa vikishuhudiwa kwenye vijiji vya Bulto, Dide Waride na Chalaluma, tarafa ya Witu na Bar’goni, tarafa ya Hindi. Hali hiyo kwa miaka mingi imekuwa ikizorotesha elimu ya mtoto msichana.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo kwenye vijiji mbalimbali vinavyokumbwa na tatizo hilo juma hili ulibaini kuwa visa vya tohara ya wasichana vinaendelea kupungua kwa kiwango kikubwa na hata kuboresha idadi ya wanafunzi wa jinsia ya kike wanaohudhuria masomo kwenye maeneo husika.

Hali hiyo inatokana na kampeni mbalimbali za kupinga ukeketaji zinazoendelezwa na machifu, wazee wa mitaa, maafisa wa nyumba kumi na jamii yenyewe kwenye maeneo husika.

Miongoni mwa mbinu ambazo zimetumika kudidimiza tohara ya wasichana kwenye vijiji vya Lamu ni kuwalenga wanawake wazee ambao ndiyo waganga au ngariba na kubadilisha hali yao ya maisha, ikiwemo kuwafadhili katika miradi ya kibiashara.

Chifu wa lokesheni ya Dide Waride, Abdi Bocha, alisema ngariba wengi kwa sasa wameacha harakati zao na kugeukia uuzaji wa maziwa, samaki na mboga.

“Tulianza kampeni zetu dhidi ya ukeketaji kwa kubadilisha maisha ya akina mama ambao kazi yao ilikuwa kutahiri wasichana wetu. Tuliamua kuwageuza kuwa wanabiashara, hivyo kukosa muda wa kufikiria kutahiri wasichana wetu. Ngariba wengi kwa sasa ni wauzaji samaki, mboga, matunda na maziwa,” akasema Bw Bocha.

Chifu wa Chalaluma, Hussein Dokota alisema hamasa mbalimbali zinazoendelea kutolewa kwa jamii zinazothamini tohara kwa wasichana pia zimesaidia pakubwa kuzika itikadi hiyo kwenye kaburi la sahau.

Bw Dokota alisema kila mara wamekuwa wakiingia mijini na vijijini ili kuwaelimisha na kuwaonya wakazi dhidi ya kujihusisha na ukeketaji.

Chifu huyo alisema mila ya kutahiri wasichana ilikuwa ikiendelezwa sana vijijini mwao hasa wakati wa likizo.

“Unapata wasichana wa kati ya umri wa miaka 10 au 14 wakipashwa tohara kisiri hasa nyakati za likizo. Machifu, wazee wa mitaa, nyumba kumi na viongozi wengine wa jamii tumekuwa tukiingia vijijini na mashuleni kutoa wosia kwa wananchi kuepuka ukeketaji. Juhudi zetu tayari zimezaa matunda kwani visa vichache vilivyoko vinafanywa kisiri au kuwe hakuna kabisa,” akasema Bw Dokota.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni dhidi ya Ukeketaji eneo la Witu, Khalif Hiribae, aliipongeza serikali kwa juhudi zake katika kuhakikisha tatizo la tohara kwa wasichana linakabiliwa.

Alisema kampeni hizo zimepelekea idadi ya wasichana wanaohudhuria masomo kuongezeka siku za hivi karibuni. Bw Hiribae aliisihi jamii kushikilia elimu na kuepuka kujihusisha na tamaduni zilizopitwa na wakati.

“Ukeketaji ni kizingiti kwa elimu ya mtoto wa kike. Punde msichana mdogo anapokeketwa, kinachofuatia ni kulazimishiwa ndoa ya mapema. Nafurahi kwamba kupitia kampeni dhidi ya ukeketaji, idadi ya wasichana wanohudhuria masomo imeongezeka kwa kiasi kikubwa eneo hili,” akasema Bw Hiribae.

Bi Fatma Dhadho aliwataka wadau zaidi kujitokeza na kushirikiana ili kupiga vita tohara ya wasichana miongoni mwa jamii, hasa zile za wafugaji.

You can share this post!

Mimi si mchawi – Raila Odinga

Shinikizo mbunge amlipe mpenzi wa zamani Sh200,000 kila...