Wanaofariki kuzikwa chini ya saa 72

Wanaofariki kuzikwa chini ya saa 72

Na SAMMY WAWERU

SERIKALI imeamuru wanaofariki kuzikwa chini ya kipindi cha saa 72.

Rais Uhuru Kenyatta alitoa amri hiyo kupitia hotuba yake kwa taifa Ijumaa.

Kiongozi huyo wa nchi alisema hatua hiyo itasaidia kuzuia watu kukongamana katika maombolezi, kama njia mojawapo kuzuia maenezi zaidi ya Covid-19.

Rais Kenyatta pia alitangaza kupunguza idadi ya wanaohudhuria mazishi kutoka waombolezaji 200 hadi 100.

Baraza la Makundi ya Kidini na ambalo lilitwikwa jukumu la kusaidia serikali kutoa mapendekezo kudhibiti msambao wa Covid-19 nchini, mwaka uliopita lilikuwa limetoa idhini ya watu 200 kuhudhuria hafla za mazishi.

“Kuhusu mazishi, yafanywe chini ya saa 72 baada ya kifo kuthibitishwa. Yahudhuriwe na watu wa familia pekee, na idadi isizidi 100,” akasema Rais Kenyatta.

Rasi pia alisema hafla za harusi zihudhuriwe na idadi ya watu wasiozidi 100.

“Maeneo ya kuabudu, yasizidi thuluthi moja ya idadi jumla,” akasema.

Wakati huo huo, Rais Kenyatta alipiga marufuku hadhara na mikusanyiko ya kisiasa kwa muda wa siku 30 zijazo, huku kafyu ya kitaifa inayotekelezwa kati ya saa nne usiku hadi saa kumi asubuhi ikirefushwa kwa muda wa siku 60 zijazo.

“Amri ya marufuku ya mikusanyiko ya kisiasa itaanzia kwangu kama Rais hadi kwa diwani (MCA). Yule ambaye atathubutu kuvunja hiyo sheria, awe ni nani ama nani atashughulikiwa kulingana na sheria za Kenya,” akaonya.

Mikusanyiko na mikutano ya kisiasa imetajwa kuchangia ongezeko la visa vya maambukizi ya corona nchini.

Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga chini ya kundi la ‘Kieleweke’ wamekuwa katika mstari wa mbele kuandaa mikutano ya umma katika mchakato wa kupigia debe Ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), huku Naibu Rais Dkt William Ruto akiongoza vuguvugu lake la ‘Tangatanga’ kupinga Mswada huo wa Mapendekezo ya Marekebisho ya Katiba 2020.

Bw Odinga amethibitishwa kuambukizwa virusi vya corona.

You can share this post!

Vinara wa EPL wanataka mashabiki 10,000 kuruhusiwa...

BETWAY CUP: Congo Boys yataka mechi dhidi ya Gor Mahia iwe...