Wanaojiita ‘mahasla’ kusukumwa jela

Wanaojiita ‘mahasla’ kusukumwa jela

Na GUCHU NDUNG’U

WAKENYA wanaojiita ‘mahasla’ wataanza kusukumwa gerezani wabunge wakipitisha pendekezo la kufanya mjadala huo kuwa haramu.

Hii ni baada ya Serikali kupitia kwa Kamati ya Usalama bungeni kupendekeza gumzo kuhusu “mahasla” lijumuishwe kati ya makosa ya uchochezi.

Hatua hiyo inafuatia kusambaa kwa mjadala kuhusu pengo la kiuchumi kati ya watu maskini (mahasla) na mabwanyenye (dynasties), ambao serikali inasema ni hatari kwa usalama wa taifa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ya bunge, Paul Koinange anasema wanataka mjadala huo kujumuishwa katika makosa ya uchochezi na ubaguzi.

Tayari mswada umeandaliwa na unatarajiwa kujadiliwa na kupitishwa na wabunge watakaporejelea vikao baadaye mwezi huu.

“Hakuna tofauti ya wananaochochea watu kwa misingi ya kikabila na wale wanaotumia suala la tabaka. Sheria inafaa kubadilishwa kujumuisha makosa haya,” asema Bw Koinange.

Naibu Rais William Ruto na wafuasi wake wamekuwa katika mstari wa mbele kusukuma mjadala huo wakidai wanatetea mamilioni ya watu maskini nchini.

Naibu Rais Dkt William Ruto abeba wilbaro juujuu huku akishangiliwa na wafuasi wake katika mkutano wa siasa awali. PICHA/ MAKTABA

Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga kwa upande wao wamekuwa wakikashifu mjadala huo na kuupuzilia mbali kama ‘takataka’.

Akiongea katika Kaunti ya Nyeri mnamo Jumapili, Rais Kenyatta aliwatania wanaoendeleza mjadala huo akisema vijana wanahitaji kazi za maana kuliko kupewa wilbaro, ambazo Dkt Ruto amekuwa akigawa maeneo kadhaa nchini.

Wakereketwa wa Dkt Ruto nao wanasema unawaunganisha Wakenya maskini bila kujali makabila wanamotoka.

“Mjadala wa ‘hasla’ sio wa kutenganishwa Wakenya mbali kuwaunganisha. Kwa mara ya kwanza tangu Kenya ilipopata uhuru kuna hisia za umoja miongoni mwa watu maskini bila kujali makabila yao. Hii ni kuhusu watu wanaopitia matatizo sawa licha ya mahali wanakotoka,” akasema Mbunge wa Belgut, Nelson Koech.

Baadhi ya wanasiasa wanasema sheria hiyo inayopendekezwa na kamati ya Bw Koinange ina lengo la kuzima kampeni za Dkt Ruto kuelekea uchaguzi wa 2022.

‘Wapinzani wetu wanapasa kukubali kuwa tuna mjadala mzuri kuliko wao na mawazo bora kuhusu jinsi ya kuwakwamua maskini kutokana na hali yao. Sijui ni kwa nini wanaogopa,” akasema Mbunge wa Soy, Caleb Kositany.

You can share this post!

BB Erzumspor anayochezea Johanna Omolo yaendelea kufufuka...

Otieno arejea kutoka Zambia kuwa kizibo cha Asieche kambini...