Habari za Kitaifa

Wanaokodi mabasi ya shule kugharamika zaidi ajali ikitokea


KUKODISHA basi la shule kwa shughuli  za kibinafsi huenda kukawa ghali endapo ajali itatokea.

Hii ni kufuatia uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu.

Jaji Roselyn Aburili amesema ni makosa kushurutisha kampuni za bima kufidia matukio ambayo hayajajumuishwa kisheria na yasiyo sehemu ya sera kati ya pande husika.

Alisema ikiwa shirika la bima litalazimishwa kufidia matukio hayo, hatua hiyo italenga pande zisizohusika kwenye mkataba na pia kukiuka sheria.

“Matokeo yatakuwa kuwapa manufaa wahusika wasiostahili na kumwadhibu anayetoa bima kupitia kandarasi ambayo haikuafikiwa,” alisema Jaji katika uamuzi uliotolewa katika mahakama ya Kisumu Agosti 2024.

Jaji alisema bodi za usimamizi wa shule zinapaswa kuarifiwa na kutoa wito kwa wanaokodishwa basi za shule kusoma sera za bima kuhusu matumizi ya mabasi hayo kabla ya kutoa hela na kuhatarisha maisha ya ‘abiria ambao hawajaidhinishwa.’

“Natumai kuwa uamuzi huu utasambazwa kwa shule zote nchini kupitia wakurugenzi wa elimu katika kaunti ili kufahamisha bodi za usimamizi wa shule, kuhusu hatari zinazohusishwa na mtindo huo, ambao tishio lake hujitokeza tu wakati kesi ya ajali inapowasilishwa na walioathiriwa,” alisema.

Jaji Aburili aliutoa uamuzi huo katika kesi iliyowasilishwa na kampuni ya Old Mutual General Insurance Kenya Limited dhidi ya bodi ya usimamizi katika Shule ya upili ya Malazi na ya Wanafunzi Spesheli ya  Oder Boys, Kisumu.

Katika kesi hiyo, waumini wa Kanisa la Seventh Day Adventist, ambao ni wafadhili wa shule hiyo, walikodi basi la shule Aprili 23, 2023, kuwasafirisha kwa hafla ya kanisa katika Kaunti Kakamega.

Basi hilo lilipata ajali katika barabara kuu ya Kisumu-Kakamega na abiria kadhaa wakajeruhiwa.

Abiria waliojeruhiwa baadaye waliwasilisha kesi kortini wakitaka kufidiwa lakini kampuni ya bima ikapinga kesi hiyo ikihoji kwamba haiwajibiki kwa sababu basi halikuwa linatumika kwa kusudi lililochukuliwa bima wakati wa ajali.