Wanaomezea mate ugavana waongezeka

Wanaomezea mate ugavana waongezeka

Na KALUME KAZUNGU

ORODHA ya wanasiasa wanaomezea mate kiti cha ugavana katika Kaunti ya Lamu inazidi kuongezeka, baada ya aliyekuwa naibu gavana, Bw Eric Mugo kutangaza azimio lake.

Bw Mugo alikuwa naibu wa gavana wa zamani, Bw Issa Timamy ambaye pia anataka kushindania kiti hicho katika uchaguzi unaotarajiwa mwaka ujao.

Waliondoka mamlakani baada ya uchaguzi wa 2017 ambapo walishindwa na Gavana Fahim Twaha wa Chama cha Jubilee, anayepanga kutetea kiti chake mwaka ujao.

Mwingine aliyetangaza azma ya kuwania kiti hicho ni mwanaharakati wa masuala ya kijamii, Bi Umra Omar ambaye atakuwa mwanamke wa kwanza kuwahi kuwania wadhifa huo Lamu.

Bi Omar, ambaye ni mfuasi wa mrengo unaoegemea upande wa Naibu Rais Wilmiam Ruto, anatarajia kuwania kiti hicho kupitia Chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Bw Mugo ambaye hajataja chama atakachojiunga nacho alisema anaamini tayari ana tajiriba ya uongozi katika kaunti hiyo.

Bw Mugo alisema lengo lake kuu ni kupigania maendeleo ya Lamu na kuinua zaidi maisha ya vijana wa eneo hilo ambao wengi wao wamepotelea kwenye janga la mihadarati.

“Azma yangu ya kupigania kiti cha ugavana ni kutaka kuhakikisha vijana wetu hapa wanasoma na kupata ajira moja kwa moja kwenye miradi ya serikali,” akasema Bw Mugo.

Alisema Lamu iko na uwezo mkubwa pia katika sekta ya kilimo ambayo anahisi bado haijatawaliwa vilivyo.

“Lamu ina kilimo cha korosho, minazi, pamba, maembe, tikitimaji na kadhalika. Wakati wa enzi yetu, tulikuwa tumeanzisha mpango wa kujenga kiwanda cha matunda pale Hongwe. Ninaamini nikiingia mamlakani nitahakikisha kiwanda hicho kinajengwa na kukamilika. Kukiwa na kiwanda, wakulima wetu watapata soko la karibu,” akasema Bw Mugo.

Kwa upande wake, Bw Timamy ambaye ni wa chama cha Amani National Congress (ANC) alisema lengo lake ni kurekebisha hali katika sekta muhimu kama vile afya.

“Wakati wetu tulikuwa tumehakikisha hospitali na zahanati zinajengwa kila mahali. Dawa pia tuliweka. Inasikitisha kwamba hospitali na zahanati hizo zimebaki kuwa majengo tu. Hakuna wafanyakazi wala dawa,” akasema Bw Timamy.

Naye Bi Omar aliwarai wakazi kumwamini licha ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwania ugavana Lamu, akishikilia kuwa atapigania vilivyo vijana kupata ajira na kuinua maisha yao.

“Wanawake pia tunaweza. Cha msingi ni jamii iniamini na kunichagua. Tayari nimefanyia jamii yangu mambo mengi. Niko tayari kutekeleza maendeleo zaidi eneo hili nikiwa uongozini,” akasema Bi Omar.

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Uchaguzi wa Zambia uwe kielelezo...

Vijana wataka vyuo vya kiufundi vianzishe masomo ya...