Wanaomezea ‘tosha’ ya Uhuru

Wanaomezea ‘tosha’ ya Uhuru

Na MWANGI MUIRURI

HATUA ya mawaziri kadhaa kujitokeza wazi kutaka mmoja wao awe rais ifikapo mwaka wa 2022, imeongeza idadi ya kambi zinazomtia presha Rais Uhuru Kenyatta kuhusu urithi wake.

Rais Kenyatta amekuwa akivutwa kila upande na mirengo tofauti ambayo kila mmoja una pendekezo tofauti kuhusu anayestahili kumrithi mamlakani baada ya uongozi wake.

Mnamo Alhamisi katika Mji wa Kangari ulioko Kaunti ya Murang’a, Waziri wa Uchukuzi, Bw James Macharia alitangaza kuwa mawaziri wameamua kumuunga mkono mmoja wao ili kukamilisha ajenda za maendeleo zilizoanzishwa na Rais Kenyatta.

“Sisi ndani ya baraza la mawaziri tumeamua huyu Dkt Matiang’i ndiye chaguo letu na tumefika ile awamu ambayo hatufichi nia yetu. haja yetu ni kumpa uongozi wa taifa hili mtu ambaye ataelewa kuhusu miradi tele ambayo tumezindua na ndio isikwame Rais Kenyatta akistaafu. Yule ambaye tumetambua ana uwezo huo ni Dkt Matiang’i,” alisema.

Tangazo sawa na hili lilikuwa limetolewa awali na Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya. Kufikia sasa, Dkt Matiang’i hajatangaza wazi ikiwa atawania urais, lakini ziara zake nyingi maeneo ya Kisii husemekana na wadadisi kwamba ni ishara analenga kujitosa katika siasa.

Bw Macharia alikuwa ameandamana na Dkt Matiang’i, Waziri wa Habari na Teknolojia Joe Mucheru na Naibu wa waziri wa Spoti Bw Zack Kinuthia.

Kuna mrengo unaojumuisha wandani wa karibu wa rais ambao huwa hawafichi nia yao kutaka urithi huo umwendee kinara wa ODM, Bw Raila Odinga. Licha ya kuwa Bw Odinga hukataa kutangaza azimio lake kuhusu 2022 wazi na husisitiza hata akiwania hatahitaji ‘tosha’ ya kigogo yeyote wa kisiasa, baadhi ya wandani wake hutaka Rais amuunge mkono 2022 kwa vile alimsaidia kudhibiti serikali yake kupitia handisheki.

Kulingana na wadadisi wa kisiasa, kuna uwezekano mkubwa pia baadhi ya jamaa za Rais Kenyatta wanampigia debe Seneta wa Baringo Bw Gideon Moi kwa wadhifa huo. Hii ni kutokana na kuwa aliyekuwa rais, marehemu Daniel arap Moi, ndiye alimshika Rais Kenyatta mkono hadi akafika mahali alipo.

Mzee Moi naye alikuwa amehudumu kama makamu wa rais katika utawala wa rais wa kwanza wa taifa, marehemu Jomo Kenyatta, ambaye ni babake Uhuru.

Kwa upande mwingine, wanasiasa walioshirikiana kwa karibu na Rais wakati wa chaguzi za 2013 na 2017 Mlima Kenya wanataka atimize ahadi yake ya kumpokeza Naibu wa Rais Dkt William Ruto mwenge wa kuongoza taifa mwaka 2022.

Vigogo wengine ambao hupigiwa upatu kumrithi Rais Kenyatta ni Kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Musalia Mudavadi (kushoto) na Kalonzo Musyoka. Picha/ Maktaba

“Hii ni mitandao iliyo na nguvu sana na huenda Rais ajipate katika hali sawa na mchezaji kamari ya pata potea,” asema Mchanganuzi wa siasa za eneo la Mlima Kenya, Prof Ngugi Njoroge.

Aliyekuwa mbunge wa Maragua Bw Elias Mbau aliambia Taifa Jumapili kuwa, endapo Bw Odinga atakuwa kipenzi cha Rais kuwania wadhifa huo, itabidi apate uungwaji mkono wa mabwanyenye wa Mlima Kenya na vile vile awe na mgombea mwenza kutoka eneo hilo.

Kulingana naye, mabwanyenye hao wamewahi kuonyesha ushawishi wao katika chaguzi kuu zilizopita na wakati huu hautarajiwi kuwa tofauti.

Aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Peter Kenneth ndiye hutajwa kama anayeweza kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga.

Nyadhifa zinazoundwa katika ripoti ya BBI zitumike kuwaleta pamoja wengine walio na ushawishi kutoka jamii za Kalenjin, Abaluhya na Wakamba ndani ya muungano huo ndio uwe na makali ya ushindani, kwa mujibu wa Bw Mbau.

Kauli hii iliungwa mkono na aliyekuwa mbunge wa Dagorretti Kusini Bw Dennis Waweru aliyepuuzilia mbali wanaoeneza dhana kuwa Bw Odinga hawezi kupata ufuasi Mlima Kenya.

“Kunao wanaosema kuwa Bw Odinga hawezi akachaguliwa. Huo ni uongo kwa kuwa Bw Odinga ni Mkenya aliye na nafasi sawa ya kuchaguliwa hata na watu wa Mlima Kenya,” akasema Bw Waweru, ambaye ni mwandani wa Rais Kenyatta.

Mtandao unaomtaka Rais kumtangaza Seneta Moi kama mrithi wake, hushikilia kuwa jamii ya Kenyatta inafaa ‘kurudisha mkono’ kwa jinsi marehemu Mzee Moi alivyokuwa mwaminifu kwao tangu akiwa makamu wa rais hadi kufariki kwake.

Mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi. Picha/ Maktaba

“Familia ya hayati Kenyatta iko na heshima kuu kwa familia ya rais wa pili wa taifa hili Marehemu Daniel Moi. Ni mzee Moi ambaye alimwongoza Uhuru hadi akamweka katika mkondo wa kushinda urais. Familia hii inaweza kurudisha mkono kupitia kwa kumuunga mkono mwana wa marehemu Moi na ambaye ni Seneta wa Baringo,” akadokezea Taifa Jumapili mmoja wa wahusika katika mtandao huo, ambaye aliomba asitajwe jina.

Mbunge wa Mathira, Bw Rigathi Gachagua ambaye ni mwandani mkubwa wa Dkt Ruto, alisema Rais hafai kujishughulisha na masuala kuhusu urithi wake.

“La busara sasa ni awajibikie kumaliza awamu yake ya uongozi na atuachie sisi hapa nyanjani tukarangane hadi tuamuliwe na raia kupitia kura na kusiwe na wa kujaribu kumhujumu mwingine,” akasema.

Mnamo Januari, Rais alidokeza hataunga mkono mgombeaji urais kutoka jamii ya Wakalenjin wala Wakikuyu, akisema ni muhimu wadhifa huo uende kwa jamii nyingine.

You can share this post!

DINI: Msalaba ndio siri ya mafanikio; hakuna utukufu bila...

Makao Makuu ya Katoliki Vatican hatarini kufilisika