Habari Mseto

Wanaomiliki bunduki haramu Samburu waonywa

December 12th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ONDIEKI

[email protected]

Serikali imetoa onyo kwa wakazi wa kaunti ya Samburu wanaomiliki bunduki kinyume na sheria kuzisalimisha mara moja kabla ya zoezi la kuzitwaa kwa lazima halijang’oa nanga.

Kamishna wa kaunti ya Samburu John Korir alisema kuwa makataa ya kusalimisha silaha hizo yalikamilika na mkazi yeyote anayemiliki silaha hatasazwa kwenye zoezi la kuwapokonya bunduki linalotarajiwa kung’oa nanga wakati wowote.

Kulingana naye, serikali itawapokonya kwa lazima wakazi ambao watakaidi amri ya kurejesha silaha hizo.

“Baadhi bado wanamiliki bunduki na nahimiza wazisalimishe tu hata kama makataa yalikamilika kwa sababu mwishowe tutawapokonya kwa lazima,” alisema Bw Korir.

Matamshi ya kamishna huyo yanajiri wakati serikali imepanga kufanya msako mkali katika maeneo ya kaskazini mwa Bonde la ufa kutwaa silaha zinazomilikiwa na wakazi kinyume na sheria.

Bw Korir aliongeza kuwa zoezi hilo halitasaza wafanyakazi wa umma, wanasiasa na viongozi wengine wenye ushawishi katika kaunti ya Samburu ambao huenda wanafadhili mashambulizi na wizi wa mifugo.

Alihimiza machifu na manaibu wao kuwa katika mstari wa mbele kupigana na wizi wa mifugo kwa sababu wanawafahamu watu vizuri katika maeneo yao.

Bw Korir alitoa wito kwa viongozi kuwashawishi wakazi kusalimisha silaha. “Tunajaribu kutwaa bunduki haramu kwa usaidizi wa machifu na maafisa wengine wa usalama hapa. Naomba viongozi watusaidie kutekeleza hilo,” aliongeza Bw Korir.

Idadi kubwa ya watu wametoroka makwao kutoka sehemu ya kaskazini ya Samburu hasa maeneo ya Baragoi, baada ya misururu ya mashambulizi na wizi wa mifugo.

Hivi majuzi viongozi kadhaa walishutumu serikali kwa hatua ya kuwapokonya bunduki polisi wa akiba katika maeneo hayo.

Lakini serikali ilitetea hatua hiyo ikisema kuwa baadhi ya polisi wa akiba walikuwa nyuma mashambulizi hayo. Zaidi ya bunduki 3,000 zilitwaliwa kutoka kwa polisi wa akiba.

Mnamo Septemba, Mshirikishi wa eneo la Bonde la Ufa George Natembeya alitangaza kuwa zoezi la kuwapokonya bunduki wakazi katika maeneo ya kaskzini mwa Bonde la Ufa litang’oa naga hivi karibuni baada ya makata kukamilika.

Kaunti ambazo zinalengwa ni pamoja na Turkana, West Pokot, Baringo, Elgeyo Marakwet, Samburu na Laikipia.